Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini zitakazoanza kutumika kuanzia leo, huku bei ya mafuta yaliyopokelewa bandari ya Dar es Salaam ikiwa imepungua kulinganisha na tole lililopita.
Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Godfrey Chibulunje, ilieleza kwamba bei hizo zitaanza kutumika leo.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba Pamoja na kutambua bei hizo, ni muhimu kuzingatia yafuatayo;
Moja, bei za jumla na rejareja za mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam zimepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la Mei 6, 2020.
“Bei za mafuta ya Taa zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la Mei 6, 2020 kwani hakuna shehena ya mafuta hayo iliyopokelewa mwezi Mei 2020 kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mwezi Juni 2020, bei za rejareja za Petroli na Dizeli zimepungua kwa sh. 348/lita (sawa na asilimia 18.65) na sh. 300/lita (sawa na asilimia 16.25), mtawalia,” ilieleza taarifa hiyo.
Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli na Dizeli zimepungua kwa sh. 347.40/lita (sawa na asilimia 19.93) na sh. 299.05/lita (sawa na asilimia 17.38), mtawalia.
Kwa mwezi Juni 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la Mei 6, 2020.
“Hii ni kwasababu kwa mwezi Mei 2020, hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Tanga,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mwezi Juni 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya Petroli katika Mikoa ya Kusini (yaani Mtwara, Lindi na Ruvuma) hazitabadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Mei 6, 2020 kutokana na kuwa hakuna shehena ya Petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.
Hata hivyo, bei za mafuta ya dizeli zimepungua ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita. Kwa mwezi Juni 2020, bei za jumla na rejareja za dizeli zimepungua kwa sh. 425/lita (sawa na asilimia 19.45) na sh. 423.24/lita (sawa na asilimia 20.58), mtawalia.
“Kwa kuwa hakuna mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium).
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote