Na Ashura Jumapili TimesMajira Online, Bukoba,
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini(EWURA),imewaonya wakandarasi na mafundi umeme,wasio kuwa na leseni kuacha kufanya kazi ya kuweka mifumo ya umeme kwenye majengo mbalimbali,kwani ni kosa kisheria nawatakaobainika watatozwa faini au kifungo.
Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa George Mhina,amesema hayo Februari 25,2025,wakati akitoa mafunzo ya siku moja kwa mafundi na wakandarasi wenye leseni za kufunga miundombinu ya umeme mkoani Kagera,yaliofanyika mjini Bukoba lengo ni kuwaelekeza madhara yanayoweza kuwapata endapo watakiuka takwa hilo la kisheria.

Pia Mhina,amewashauri wananchi wa Mkoa wa Kagera,kutumia mafundi na wakandarasi wenye leseni zinazotambuliwa na mamlaka hiyo, pindi wanapotaka kufungiwa miundombinu ya umeme kwenye nyumba zao, ili kuepuka adha za kupoteza mali,vifo na kutapeliwa na watu wasiowaaminifu.
Amesema,mamlaka hiyo inapata kesi nyingi kutoka kwa wananchi hasa za kupoteza nyumba zao kwa kuungua moto kutokana na itilafu ya umeme na ikichunguzwa wanagundua makosa yanatokana na utendaji mbovu na vifaa visivyo na viwango vinavyofungwa na baadhi ya mafundi wasio na leseni.
Amesisitiza kuwa ili kuhakikisha hilo linafanikiwa kwa nchi nzima wapo mafundi wenye leseni zilizotolewa na EWURA kwa mujibu wa sheria zaidi ya 6,000.Huku kwa Kanda ya Ziwa wapo 497 kati yao Mkoa wa Kagera wapo 147.Hivyo wananchi watawatambua kupitia tovuti ya EWURA kwenye sekta ya umeme na kufungua kiunganishi (link) ya wakandarasi wamo wote.
“Tunawataka Tanesco kwa kila Mkoa na Wilaya, kubandika orodha ya mafundi wote wenye leseni, hii itasaidia kupunguza vishoka na kuacha kutumia mafundi wasio na leseni ambao husababisha matatizo ikiwemo nyumba za wateja kuungua na hasara zisizo tarajiwa,”amesema Mhina.
Sanjari na hayo,amewatahadharisha wakandarasi wenye leseni kutotumia mihuri yao katika kazi ambazo hawajafanya, ikigundulika kuwa mhuri huo au leseni vilitumika kwenye ile kazi na likitokea janga anakamatwa huyo fundi ambaye anaonekana alijaza hiyo fomu ya Tanesco.
Amesema kama kuna adhabu yoyote ama kifungo au faini atausika yeye ambaye namba yake ya ukandarasi au mhuri wake vilitumika katika fomu ya kuombea umeme Tanesco
Mwanasheria wa EWURA kutoka Dodoma, Baraka Butoto,amesema wakandarasi na mafundi umeme,wasiokuwa na leseni kwenye mamlaka hiyo,wachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwemo kifungo cha miaka mitano au faini isiyozidi milioni moja.
Kwa upandea wake,Ofisa Uhusiano Huduma kwa Wateja Tanesco Mkoa wa Kagera,Lilian Mungai,amesema shirika hilo linafanya jitihada za kukabiliana na tatizo la vishoka,matapeli,wakandarasi na mafundi wasio na leseni kwa kuanzisha utaratibu mpya unaitwa nikonekti.

Amesema utaratibu huo una uwazi ambapo kila mtu ambaye anahitaji kufungiwa umeme anaweza kufanya maombi yake kupitia simu yake ya mkononi au kompyuta kwa kuingia katika tovuti ya nikonekti.
Mmoja wa wakandarasi walihudhuria mafunzo hayo Rwagaya Buberwa,amesema changamoto ya kufungiwa umeme na nyumba ikapata itilafu na kuungua inatokana na watoa huduma zaidi ya mmoja ikiwemo wale ambao hawajathibitishwa na EWURA.
Hivyo amewashauri wakandarasi na mafundi wenye sifa kuomba leseni ambayo ni takwa la kisheria, ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi bila kukabiliwa na changamoto za kisheria pindi wanapotekeleza majukumu yao.

More Stories
Dkt. Matarajio: Tunataka Nishati ya Petroli iwe injini ya maendeleo
Wanahabari wataka magari maalum misafara ya viongozi
TAKUKURU Gairo waja na kliniki tembezi kutoa elimu ya kupambana na Rushwa