March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yawafikia wananchi 300, maonesho ya Nane Nane Kanda ya Ziwa Magharibi 

*Yapokea malalamiko yanayohusu nishati ya umeme na maji

*Yatatua papo kwa papo baadhi ya malalamiko

Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji(EWURA), Kanda ya Ziwa,imesema kupitia maonesho ya Wakulima Nane Nane,imewafikia wananchi zaidi ya 300 wakiwemo wenye malalamiko mbalimbali kuhusu huduma ya nishati ya umeme na maji.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa,George Mhina,wakati akizungumza na waandishi wa habari Agosti 8,2025, katika kilele cha maadhimisho ya Nane Nane,yaliofanyika kwa Kanda ya Ziwa Magharibi Nyamoh’ongolo, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Ambapo amesema,katika maonesho hayo EWURA iliweza kutembelewa na wananchi katika banda lao na kupata huduma mbalimbali ikiwemo elimu wastani wa watu 40 hadi 50, hivyo imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 300 katika siku nane za maonesho hayo.

Mhina amesema,wananchi waliotembelea banda hilo wapo ambao walikuwa na malalamiko yanayohusiana na masuala ya ankara za maji(bill).

Huku wengine waliomba kuunganishiwa huduma ya nishati ya umeme kwa muda mrefu na wamecheleweshewa kuwekewa nishati hiyo.

“Yapo malalamiko ambayo tuliweza kuyatatua hapa hapa katika maonesho ya Nane Nane,lakini yapo mengine ambayo kuanzia wiki ijayo tutaanza kuyafanyia kazi,”amesema Mhina na kuongeza:

“Tulipata wageni wengi katika banda letu la EWURA,na tumekutana na watu wa kawaida ambao pengine wasingeweza kufika katika ofisi zetu zilizopo katikati ya mji.Pia kupitia maonesho haya tumekutana na watu wa aina zote ikiwemo wenye uchumi mkubwa,wa kati na hata wenye uchumi mdogo,”.

Pia amesema,kupitia maonesho hayo na malalamiko yaliojitokeza Kuna haya ya mamlaka hiyo kukutana na watia huduma kwa wananchi TANESCO na mamlaka za maji.

“Tutakutana na watia huduma kwa wateja na wanasheria wao,kabla ya kuisha mwezi Septemba,kwa sababu kuna mambo ambayo yangeweza kufanyika na kuhitimishwa pasipo kuja EWURA,pengine wameshindwa kujibiidisha zaidi au hawajui taratibu zaidi wanashindwa kuwahudumia wananchi hao kwa ukaribu na matokeo yake yanakuja kwetu,”amesema Mhina na kuongeza:

“Tutakutana kwa semina elekezi na kuelimishana kabla ya mwezi Septemba mwaka huu,kwa TANESCO na mamlaka za maji siyo tu Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA), bali mamlaka zote za maji Kanda ya Ziwa,ili kukumbushana wajibu wetu wa kufanya katika kuwahudumia wateja,”.

Sanjari na hayo Mhina,amesema,kupitia maonesho hayo wameweza kutekeleza moja ya jukumu la EWURA la msingi la kutoa elimu kwa wananchi.