December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yatoa mafunzo kwa Mamlaka za maji

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

ILI kuhakikisha Mamlaka za maji zinajiendesha kwa ufanisi na kutoa huduma kwa wananchi, Mamlaka ya Udhibithi wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa imetoa mafunzo kwa Mamlaka za maji 6 za Wilaya kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya namna ya kuandaa mpango wa biashara kwa Mamlaka hizo.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa siku tano katika ofisi za EWURA Kanda ya Ziwa zilizopo Mkoa wa Mwanza, zilizoshiriki Mamlaka kutoka Wilaya ya Karagwe, Kasulu, Kibondo, Sengerema, Kishapu na Maganzo.

Akizungumza wakati wakihitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa EWURA, Mhandisi Exaud Maro amesema, walichagua mamlaka hizo kwa vile hazikuwa na mpango wa kujiendesha kama vile inavyotakiwa na sheria namba 5 ya Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019, ambayo unataka kila mamlaka ya maji na Usafi wa mazingira nchini kuwa na mpango wa kujiendesha na kama ilivyotajwa na sheria unaitwa mpango wa kibiashara.

“Watu wamekuwa wakisema kuwa hizi ni mamlaka za kibiashara hapana ni zinatoa huduma za maji na usafi wa mazingira katika miji hiyo,lakini uendeshaji wake unatakiwa uwe endelevu kama ulivyo ainishwa kwenye sheria kwa namna ya kibiashara kwa lengo la huduma kuwa endelevu,serikali yetu imewekeza sana katika mamlaka hizi ambazo zinamilikiwa kwa asilimia 100, na serikali na ili iwe endelevu lazima mamlaka hizi kujiendesha kibiashara kwa maana ya kutoa huduma ya maji na usafi wa mazingira pale ambapo wananchi wanachangia na siyo kulipia huduma kamili,” amesema Mhandisi Maro.

Amesema, ingekuwa ni mtu binafsi basi bei za maji zingekuwa mara 7 ya bei iliopo sasa kwa maana ya kuwa sasa uniti moja ni sawa na lita 1000 pia sawa ndoo 50 za lita 20 za maji kuuzwa kwa wastani wa 1,200 ila ingekuwa ni mtu binafsi pengine angeuza kwa zaidi ya 6,000 hivyo jukumu la mamlaka hizo ni huduma inayotolewa iwe endelevu kwa uendeshaji na matengenezo kwa wananchi kulipia mambo mengine ambayo yapo ndani ya matengenezo na uendeshaji maana serikali imewekeza fedha nyingi ambazo wananchi hawawezi kuzilipa.

“Huduma hizi ziwe endelevu na kuongeza idadi ya watu kuwa na mabomba nyumbani mamlaka hizo zinabidi zijiendeshe kibiashara kwa kuweza kutoza bei zinazokubaliwa na mamlaka za nchi zinazosimamiwa na Ewura,kwanza kwa kuandaa mpango wa kibiashara zizingatie gharama halisi na halali za uendeshaji na matengenezo katika kipindi cha miaka mitatu mitatu na kila mwaka watakuwa wanaainisha kazi wanazokwenda kufanya na wao kama EWURA na kuhakiki ili wananchi wapate bei halali na mamlaka hizo zijiendeshe kiufanisi,” amesema Mhandisi Maro.

Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa George Mhina amesema kuwa, mafunzo hayo yalikuwa mahususi kuhusu uandaaji wa mpango wa biashara ambapo EWURA wanatengeneza muongozo ambao mamlaka za maji watautumia na kufahamu namna ya kuandaa mpango wao wa biashara.

Mhina amesema, lengo ni baada ya mafunzo hayo mamlaka hizo ziende kuandaa mpango wao wa biashara,wawe na dira,maudhui lakini pia waweze kuboresha huduma kwenye maeneo yao,kwani serikali inajitahidi katika kuwekeza kwenye miradi ya maji na mwisho wa siku ni kumtua ndoo mama kichwani na kupata maji safi na salama.

“Tuliamua kuandaa muongozo kwa mamlaka hizi za maji ili wawe na mipango yao ya biashara, faida na maudhui yake ni kama ramani ya kuwawezesha kupanga na kujua wapi wanahitaji kuwekeza,kwani Mamlaka hizo ni ndogo na zinauza maji kwa bei ya chini kwani zipo zinazouza uniti moja ya maji sawa na ndoo 50 za lita 20 kwa shilingi 300, hivyo zinashindwa kujiendesha,kujipanua pamoja na kutoa elimu na huduma bora kwa wateja kwa vile hawana mpango wa biashara,” amesema Mhina.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Meneja Utawala na Biashara wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Sengerema Mussa Malimi, amesema mafunzo hayo yanatija ambapo yamewasaidia kwenda kuandaa mpango wa biashara ambao itasaidia kupata bei ya maji ambayo ni halali na halisi na wananchi wataweza kumudu huku wao wakiweza kujiendesha na kuwa chanzo cha kujiinua na kuboresha huduma za maji kwa kwani lengo ni kutoa huduma bora za maji safi kwa watu huku ili kuongeza idadi ya wateja watato elimu kwa wananchi ili waweze kuunganishiwa maji na kupata huduma ya maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.