March 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yaendelea kuweka mazingira rafiki ya biashara ya gesi

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mkurugenzi wa Gesi Asilia wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Poline Msuya, amesema EWURA inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuhamasisha uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa biashara ya gesi asilia iliyogandamizwa (CNG) ikiwa ni hatua muhimu katika kusaidia juhudi za Serikali za kuchochea matumizi ya nishati safi nchini.

Msuya ameyasema hayo wakati wa majadiliano ya jopo katika mkutano wa awali wa Mkutano wa 11 wa Mafuta na Gesi wa Afrika Mashariki (EAPCE’25) uliofanyika leo tarehe 04.03.2025 jijini Dar es Salaam. Mkutano husika ambao ni wa siku tatu utaanza rasmi kesho tarehe 05.03.2025.

Ameeleza kuwa moja ya hatua muhimu zilizokwisha kuchukuliwa kuhamasisha uwekezaji ni pamoja na kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye miundombinu muhimu ya CNG, ikiwa ni pamoja na mashine za kushindilia gesi (compressors), vitengo vya kupima gesi (metering units), na hifadhi za CNG (storage cascades) jambo linalovutia uwekezaji zaidi katika sekta husika.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo zaidi ya magari 7,000 yamefungwa mfumo wa gesi ili kuyawezesha kutumia gesi ya (CNG) inayopatikana kwenye vituo mbalimbali nchini hususan Dar es Salaam huku zaidi ya vituo 10 vipya vya CNG viko mbioni kujengwa.

Amesema mwamko wa wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo ya ujenzi wa vituo vya gesi za magari CNG umeongezeka na kuwa ongezeko hilo limeonekana pia kwenye kubadilisha mfumo wa magari wa kutumia petroli na kuwa gesi.

“Mwitikio ni mkubwa, Watanzania wanachangamkia fursa, na sisi EWURA ndio tunatoa vibali vya ujenzi wa vituo hivyo vya CNG , tunaona mwitikio, na idadi ya magari imeongezeka kutoka 2,000 miaka michache iliyopita hadi kufika magari zaidi ya 7,000 sasa,”amesema Kaguo.

Amesema wapo wawekezaji wengi wameonesha nia ya kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya CNG na kuwa EWURA wanapopokea maombi, wanayashughulikia mapema ili kuhakikisha ujenzi wa vituo hivyo unafanywa.