Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kupanda kwa bei za mafuta itakayoanza kutumika kesho.
Kwa Dar es Salaam, Petroli imepanda kutoka Sh. 1693 hadi Sh. 1832, Tanga kutoka Sh. 1654 hadi 1868, Mtwara kutoka Sh.1612 hadi 1875 huku kwa upande wa Dizeli kwa Tanga ikipanda kutoka Sh. 1693 hadi 1778 na Mtwara kutoka Sh. 1731 hadi 1799.
Licha ya kupanda kwa bei hizo za za mafuta imeelezwa kati ya Meli sita za petroli zilizotarajiwa kuingia nchini kuanzia Julai 29 hadi Agosti 31 mwaka huu, tayari Meli tatu zimewasili nchini zikiwa na jumla ya lita milioni 89.564 kwa ajili ya soko la ndani .
Kiasi hicho kitatosheleza mahitaji ya nchi kwa zaidi ya siku 18 huku Meli tatu nyingine zikitarajiwa kuwasili kati ya Agosti 17 na Agosti 31 mwaka huu zikiwa na lita takribani milioni 100.075 zitakazotosheleza mahitaji ya nchi kwa zaidi ya siku 22.
Akizungumza leo na waandishi wa Habari jijini Dodoma, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Titus Kaguo amesema, mafuta ya dizeli yapo ya kutosa na Meli tatu za mafuta hayo zenye jumla ya lita milioni 193.391 zinategemewa kuingia nchini Agosti mwaka huu .
Kaguo amesema,kiasi hicho cha mafuta hayo yatatosheleza mahitaji kwa zaidi ya siku 30 na ili kuwa na utoshelevu wa mafuta nchini, kuanzia Septemba mwaka huu, EWURA imeongeza makadirio ya matumizi ya mafuta kwa siku kuwa lita milioni 4.812 kwa petroli na lita milioni 6.082 kwa dizeli.
Akitoa ufafanuzi juu ya changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini kuanzia mwishoni wa Julai, Kaguo amesema, jambo hilo limechangiwa na kuchelewa kwa meli moja iliyokuwa ifike nchini kati ya Julai 22 na 24 na badala yake iliingia nchini Julai 29.
Sababu kubwa zilizoelezwa kusababisha mecli hiyo kuchelewa ni kutokana na changamoto zilizokuwepo ikiwemo upepo wa ‘Monsoon’ baharini na kufanya meli kusafiri kwa kasi ndogo lakini Mamlaka hiyo ilifanya kila jitihada za kuhakikisha mafuta yanapatikana maeneo yote nchini.
Amesema, wamehakikisha na wataendelea kuhakikisha kuwa usambazaji wa mafuta hapa nchini unaendelea kuwa wa kuridhisha kama kwa ilivyo sasa na ambapo upatikanaji wake ni wakuridhisha kwani maeneo yote yana mafuta ya kutosha isipokuwa maeneo machache.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba