November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA

EWURA kufuta leseni kampuni tano za mafuta

Na David John, TimesMajira Online, Dar Es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) inatarajia kufuta leseni tano za wauzaji wa mafuta ya jumla na rejareja kutokana na kukiuka taratibu za leseni za utoaji wa huduma ya mafuta nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za mamlaka hiyo Dar es Salaam, Meneja wa Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo amesema kampuni hizo zimekiuka taratibu za utoaji huduma na tayari wamewasiliana nazo na kutoridhishwa na maelezo yao.

Kwa mujibu wa Kaguo, kampuni za uuzaji wa mafuta ya rejareja ambazo zitachukuliwa hatua ni B45 ya Bagamoyo mkoani Pwani, Kampuni ya Maxson Energy Limited ya Njombe, Maxson Energy Limited ya Makambako na kampuni Olmpic Petroleum.

Kwa upande wa kampuni ya uuzaji wa mafuta ya jumla, Kaguo amesema ni Mansuri Industry Limited. Kaguo alitaja kampuni nyingine kuwa ni Camel Tanzania, Morgas, ambapo kampuni ya Olmpic Limited wanakusudiwa kuifutia leseni.

Pia amemtaja muuzaji wa rejareja kutoka kampuni ya Mtweve ya wilayani Chunya kuwa anatakiwa kulipa faini ya sh.milioni sita na baada ya kulipa fedha hizo, atakwenda TRA kumalizana nao suala la kodi na kupandisha bei ya mafuta na baada ya kukidhi masharti hayo watamfungulia.

Kaguo amesema Kampuni ya Star Oil itachunguzwa kutokana na mfumo wa jinsi anavyopata mafuta, ambapo mamlaka ilijiridhisha na hoja yake, lakini Kampuni ya Morgan wao walifunga kituo baada ya kuzuiwa na Wakala wa Vipimo bila kutoa taarifa EWURA, hivyo kutokana na kosa hilo Mamlaka inakusudia kufuta leseni.

Ameongeza kuwa kampuni ya Oryx yenyewe ilitoa malalamiko ya tatizo la mfumo wa upatikanaji wa mafuta, hivyo kampuni hiyo imepewa onyo. Hata hivyo aliwataka wanunuzi wa mafuta kununua mafuta kutokana na mahitaji yaliyopo, kwani kuchukua ziada ni kusababisha uhaba wa mafuta.