April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA kinara uhusiano mwema na vyombo vya habari nchini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeshinda tuzo ya Uhusiano Mwema na Vyombo vya habari nchini, kwa mwaka 2024,ikiwa ni mara ya pili mfululizo.

Hiyo ikidhihirisha namna taasisi hiyo inavyothamini ushirikano na uhuru wa vyombo vya habari katika kuhabarisha umma kuhusu shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji.

Tuzo hiyo imetolewa Machi 29,2025 na Chama cha Maofisa Uhusiano Tanzania (PRST), baada ya mchuano uliohusisha taasisi nyingi imeipa EWURA heshima na ari ya kuendelea kudumisha uhusiano wake thabiti na vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari nchini.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo,amesema ushindi huo kwa mara ya pili mfululizo ni kielelezo cha utawala bora, uwazi, uwajibikaji na miongozo inayotolewa na Bodi na Menejimenti ya mamlaka hiyo chini ya Mwenyekiti Prof. Mark Mwandosya na Mkurugenzi wake Mkuu, Dkt. James Mwainyekule.

Amesema vigezo vilivyotumika kuipatia EWURA ushindi huo ni kuwa na mpango mkakati bora wa ushirikishwaji wa vyombo vya habari, ubora wa maudhui na uthabiti wa utoaji taarifa pamoja.

Hata hivyo Janeth Mesomampya, ambaye ni Ofisa Uhusiano wa EWURA amepokea tuzo ya Ofisa Uhusiano bora kwa mwaka 2024, akiwa mmoja wa washindi watano katika kipengele hicho.

Wilfred Mwakalosi (kushoto), Ofisa Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano EWURA akipokea tuzo kutoka kwa Bakari Machumu, moja ya majaji wa tuzo za PRST kwa mwaka 2024, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam,Machi 29,2025

Rais wa PRST Assah Mwambene,amesema utoaji wa tuzo hizo ni chachu kwa wataalam walioko kwenye kada hiyo kufanya kazi zao kwa ubora zaidi ili kuimarisha huduma katika maeneo yao ya utendaji.

EWURA ilipata tuzo ya aina hiyo pia kwa mwaka 2022, iliyotolewa na PRST kutambua mchango wake katika kushirikiana vyema na vyombo vya habari nchini.