
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) limetakiwa kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo ya vijijini, ili kuwawezesha kuelewa haki zao na namna ya kushughulikia changamoto za huduma hizo muhimu.
Wito huo umetolewa leo Agosti 5,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alipotembelea banda la EWURA CCC katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Senyamule amesema ni muhimu kwa wananchi wa vijijini kupata elimu ya moja kwa moja kuhusu matumizi sahihi ya nishati na maji, ufuatiliaji wa bei, pamoja na mbinu bora za kutatua malalamiko dhidi ya watoa huduma.
“Tunahitaji kuona wananchi, hasa wa vijijini, wakipata uelewa wa huduma hizi kwa kuwa ndio nguzo ya maendeleo ya kilimo na biashara,” amesema Senyamule.
Aidha , Senyamule amepongeza juhudi za EWURA CCC na kuhimiza matumizi ya teknolojia salama na ufuatiliaji wa huduma, akisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kupunguza gharama za uzalishaji na kuimarisha ustawi wa jamii.
Katika maelezo yake kwa Mkuu wa Mkoa, Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa EWURA CCC, Lugiko Lugiko, amesema ushiriki wa baraza hilo kwenye maonesho ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia wananchi walioko pembezoni ambao mara nyingi hukosa taarifa sahihi za huduma wanazotumia.
“Tunatumia jukwaa la Nanenane kutoa elimu kuhusu bei sahihi za mafuta, matumizi ya gesi asilia, pamoja na jinsi ya kushughulikia bili zisizoeleweka,” amesema Lugiko.
Aidha, Lugiko ameongeza kuwa EWURA CCC inalenga kuwajengea uwezo wakulima, wanawake na vijana ili kutumia huduma za nishati na maji kuongeza thamani ya mazao yao kupitia teknolojia rafiki kwa mazingira.
EWURA CCC imeahidi kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia Watanzania wengi zaidi, hususan wale wa maeneo ya pembezoni, kwa lengo la kuboresha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora katika sekta za nishati na maji.
Wananchi waliotembelea banda la EWURA CCC wameonyesha kuridhishwa na elimu waliyoipata. Grace Ntembo, mkulima kutoka wilaya ya Busega, alisema kupitia EWURA CCC tamejua sasa namna sahihi ya kushughulikia changamoto za maji na umeme vijijini.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi