November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ETDCO Yatengeneza Faida ya Shilingi Bil. 9.6

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampuni tanzu ya Tanesco ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (Electrical Transmission and Distribution Construction and Maintenance Company, ETDCO) imetengeneza faida ya jumla ya shilingi Bil. 9.6 katika kipindi cha miaka Mitano.

Kaimu Meneja ETDCO, Mhandisi Maclean Mbonile amesema hayo katika taarifa yake ya mafanikio ya ETDCO katika miaka 60 ya Uhuru, leo Novemba 24, 2021, Jijini Dar es Salaam.

“Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2021, ETDCO imetengeneza faida ya jumla ya shilingi Bil. 9.6 tangu kuanzishwa kwake, Julai 17, 2016 ” alisema Mhandisi Mbonile.

Aliendelea kusema kuwa, ETDCO imetimiza lengo la kuanzishwa kwake, ambapo Serikali ilianzisha kampuni hiyo kwa lengo la kubuni, kusanifu na kutekeleza miradi na kuwezesha kampuni kukua na kujiendesha kibiashara.

Mhandisi Mbonile, ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kuwa ni pamoja na kutekeleza jumla ya miradi 74 yenye thamani ya shilingi Bil. 156.03. Miradi hiyo ni pamoja na, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye uwezo wa 132kV kutoka Mtwara hadi Lindi wenye thamani ya shilingi Bil. 11.4, ambao ulikamilika mwaka 2017.

Miradi mingine ni ujenzi wa njia ya kupeleka umeme yenye uwezo wa 33kV kutoka Mahumbika hadi Ruangwa, wenye thamani ya shilingi Bil. 8.7, ambao ulikamilika mwaka 2018. Ujenzi wa njia ya kupeleka umeme kwenda mji wa Serikali Mtumba na Ikulu ya Chamwino, njia ya kilomita 51 ya uwezo wa 33kV, wenye thamani ya shilingi Bil. 3.4, ambao ulikamilika mwaka 2020.

Miradi inayoendelea kutekelezwa na ETDCO mpaka sasa ni pamoja na mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa II mikoa ya Mbeya na Katavi, ambayo inahusisha kupeleka umeme kwenye jumla ya vijiji 194, ambao unathamani ya shilingi Bil. 64.5 unaotakiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.

ETDCO ilianzishwa Julai 17, 2016 na kusajiliwa na BRELA Juni 7, 2017. ETDCO inamilikiwa na TANESCO kwa asilimia 100. Malengo ya kuanzishwa kampuni hiyo, ni pamoja na kuwezesha nchi kujitegemea na kupunguza gharama za kuajiri wataalam kutoka nchi za nje; kuchangia ufanisi katika utendaji wa kampuni mama kwa kutekeleza miradi kwa uharaka, ubora, na gharama nafuu; kuridhisha wateja kwa ubora wa kazi za ujenzi na ukarabati wa miundombinu kwa ajili ya umeme wa uhakika; na kubuni, kusanifu na kutekeleza miradi na kuwezesha kampuni kukua na kujiendesha kibiashara.