December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ENVIROCARE kuendelea kutoa elimu ya Lishe na Ujumuishaji wa kijinsia mikoa ya Mbeya,Songwe

Na Penina Malundo, Timesmajira

SHIRIKA la ENVIROCARE limesema kuwa limejipanga kuendelea kutoa elimu ya Lishe na kuhakikisha linafika katika vijiji ambavyo bado havijafika vya Mkoa wa Mbeya na Songwe ili kutoa elimu kamili ya masuala ya Lishe na kupunguza hali ya udumavu.

Akizungumza hayo jana,Mkoani Mbeya Meneja wa Mradi wa Passport to Coffee Export (PACE) ambao ulianza mwaka 2020 ,Amos Mbwambo, chini ya Kampeni ya elimu ya lishe na ujumuishaji wa masuala ya kijinsia katika mkoa wa Mbeya, wilaya ya Mbeya, na mkoa wa Songwe, wilaya ya Mbozi.

Alisema Shirika lao limeanzisha Kampeni hiyo , inayofanyika kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), ambayo ni sehemu ya mwaka wa mwisho wa mradi kwa kuhakikisha watu wa mikoa hiyo wanapata uelewa wa kutosha juu ya masuala ya Lishe pamoja na Ujumuishaji wa kijinsia.

Amesema Shirika limekuwa likishirikiana na Serikali bega kwa bega katika kuhakikisha elimu hii inawafikia watu mbalimbali kupitia maafisa Lishe,Maendeleo ya Jamii pamoja na mawakili wa Serikali ili kutatua changamoto ya wanawake kumiliki Ardhi, migogoro ya ndoa, Mirathi pamoja na udumavu kwa wananchi.

“Mradi huu tunatekeleza kazi zake ndani ya mkoa wa Mbeya, Songwe, na Ruvuma, na kote huko elimu hii itawafikia na Kampeni hii inalenga kupunguza udumavu na kuongeza uelewa wa masuala ya kijinsia na sheria na kuhakikisha inaboresha hali ya maisha ya wakazi wa maeneo husika,”amesema.

Aidha Mbwambo amesema Envirocare kwa kushirikiana na serikali wameweka mikakati madhubuti kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Akitaja sababu iliyowafanya kupeleka Kampeni hiyo katika mikoa hiyo alisema kampeni hiyo imekuja baada ya utafiti walioufanya mwaka 2021 kubaini kiwango kikubwa cha udumavu na usawa wa kijinsia kuwa tatizo kubwa katika maeneo hayo.

Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Isuto, kijiji cha Itete, Ezekia Soda, amesema changamoto kubwa imeonekana kuwa ukosefu wa elimu kuhusu lishe ndio kubwa licha ya mkoa huo kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula.

Amesema pia , ukosefu wa elimu ya sheria umeonekana kuwa changamoto kubwa, ambapo inapelekea kuwepo kwa kesi nyingi zikiwemo kesi za ardhi, mirathi, na talaka.

Naye David Mwampalala, Mwenyekiti wa Kijiji cha Itete, ameishukuru Serikali kupitia shirika la ENVIROCARE, kwa namna walivyonufaika na elimu kubwa ya masuala ya Lishe na sheria ambazo zimeweza kuwaletea matumaini mapya.

“Wananchi wa kijiji chetu wamenufaika sana na elimu hii kubwa, kwani hapo awali kesi zilikuwa nyingi na sasa anaamini zitapungua kama siyo kuisha kabisa.”amesema.

Jostina Mwasinde, Mkazi wa kijiji cha Itete, ambaye alikuwa mhanga wa mgogoro wa mirathi, alionyesha shukrani zake kwa ujio wa Envirocare. “Tatizo langu limepata ufumbuzi baada ya kupatiwa elimu ya sheria mbalimbali zinazonilinda na kunitetea kama Mtanzania,” amesema Jostina.