Na John Bera, Same
NAIBU Waziri wa Malialisi na Utalii, Mary Masanja amesema Serikali imeanza kutoa elimu kwa wananchi namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kupitia wataalamu wa masuala ya wanyamapori ikiwa lengo ni kulinda usalama wa wananchi na mali zao.
Naibu Waziri Masanja ametoa kauli hiyo leo katika kijiji cha Maore kilichopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wakati akizungumza na wakazi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakikumbwa na uvamizi wa tembo katika maeneo yao.
’’Serikali inasikitika inapoona wananchi wake wanateseka na wanyamapori wakali kama vile tembo,tumetafuta mbinu mbadala ya kuhakikisha wananchi mnafundishwa namna bora ya kukabiliana na wanyamapori hawa,”amesisitiza Masanja.
Amesema, mbali ya kutolewa kwa elimu hiyo ya kukabiliana na wanyamapori hao, Serikali itagawa vifaa maalum kwa ajili ya kuwafukuza tembo wanapofika katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuwapatia namba ya simu za askari watakaokuwa wakipatiwa taarifa pale tembo wanapovamia maeneo yao ili waje kutoa msaada kwa haraka kabla tembo hawajasababisha madhara kwa wananchi.
Katika hatua nyingine,Naibu Waziri Mary Masanja amesema, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi itatenga maeneo maalumu kwa ajili ya mifugo ili kuepusha wananchi kukumbwa na changamoto ya kuharibiwa mali zao.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti