May 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu ya kilimo tija yawafikia wakulima mikoa mitano.

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa

MRADI wa Kilimo na Lishe Tanzania (NOURISH -Tanzania), umelenga kuwafikia wakulima 168,000 katika mikoa mitano nchini,ambao umelenga kuwaelimisha kuhusu kilimo cha tija ili kuleta mapinduzi kwenye sekta hiyo.

Elimu hiyo imejikita katika kuelimisha wakulima hao kuhusu usalama wa chakula, lishe bora, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi na mbegu bora.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Matai Asilia na Mkowe, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa , Ofisa wa Mradi wa NOURISH, Fikilio Gambi,amesema tangu mradi huo uanze mwaka jana umewafikia wakulima 13,556 katika mikoa ya Rukwa na Songwe kwa kutoa elimu kwa wakulima hao na jamii nzima.

Ambapo,mikoa mitano itakayonufaika na elimu hiyo ni pamoja na Dodoma, Manyara, Rukwa, Singida na Songwe.

Amesema wakulima hao wamefundishwa elimu ya lishe,kilimo chenye tija, usafi binafsi na usafi wa mazingira pamoja na kushiriki katika miradi mbalimbali ambayo itawasaidia kuongeza kipato.

Pia amesema mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo Norway (Norad) na kutekelezwa na wadau wa maendeleo SNV pamoja na Farm Africa kupitia washirika wake RECODA na MIICO.

Sambamba na hayo wakulima hao watapata fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye mashamba ya mfano yaliyofanikiwa, kuunganishwa na biashara za kilimo.

“Mradi wa NOURISH wilayani Kalambo umefanikiwa kuelimisha wananchi jinsi ya kuanzisha mashamba darasa 195 kwa mazao ya mtama,maharagwe na alizeti kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo pia kuwaunganisha wakulima na kampuni za pembejeo bora za kilimo (mbegu na viatilifu ),” amesema Gambi.

Ameongeza kuwa mradi ho umeanzisha vikundi 130, vya kilimo pia wakulima wamepewa pembejeo za kilimo kwenye mashamba darasa na kugawa kilogramu za mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia kilogramu 2,458, mbegu bora kilo 760,viatilifu lita 130 na viuakuvu kilo 65.

Ofisa KilimoWilaya ya Kalambo,Jonathan Leza amewataka washiriki wa mradi huo kuwa chachu ya maendeleo na watekeleza kwa vitendo kwenye kaya zao yale waliyofundishwa lakini pia washirikishe wanavikundi wengine elimu hiyo.

Katika mikoa hiyo mitano Mradi wa NOURISH kwa mwaka mmoja umeleta mafanikio kwa wakulima zaidi ya 6,000 wameunganishwa na wasambazaji wa pembejeo, watoa huduma 472 wa afya ya jamii wamefundishwa kuhusu lishe bora, na zaidi ya wakulima viongozi 400 wamepata mafunzo ya kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.