Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online
WAKATI Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam yakiendelea, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kutatua kero mbalimbali za wanachama na wadau waliotembelea banda hilo.
Mmoja ya wanachama aliyetembelea banda la NSSF, Bahiru Gwimile, amesema alijiunga na NSSF kupitia sekta isiyo rasmi akawa anajiwekea akiba kila mwezi, lakini baadaye alipata kazi ambapo aliendelea kuitumia akaunti yake ile ile mpaka mkataba wake wa ajira ulipomalizika na sasa ameamua kujichangia tena kupitia sekta isiyo rasmi.
“Nahamasisha vijana wenzangu, makundi mbalimbali na watu wote ambao hawajajiunga na NSSF wajiunge kwa sababu unapojiwekea akiba NSSF kuna faida ambazo utanufaika nazo baadaye kama kupata pensheni ya uzeeni ambayo itakufanya ufurahie maisha mazuri ya uzee wako,” amesema.
Kwa upande wake, Afisa Mafao Mwandamizi wa NSSF, Stella Kabyemera, amesema NSSF ilianza kutoa huduma kwa wanachama na wadau katika maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” kuanzia Juni 28,2021 na wataendelea kutoa huduma mpaka Julai 13, mwaka huu, katika banda namba 13 la mashirikiano baina ya PSSSF na NSSF.
“NSSF kupitia maonesho haya inatoa elimu ya hifadhi ya jamii, inatatua kero mbalimbali kuhusu mafao, baadhi ya wanachama wamepata huduma ya kuangalia taarifa za michango yao na kwa wale wanachama ambao hawajapata kadi zao za uanachama tunawaomba watembelee banda letu ili waweze kupata kadi zao.”
NSSF inatoa huduma zake zote zinazopatikana kwenye ofisi zake mbalimbali nchi mzima, pia wanatoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kama wajasiriamali, wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo, mama lishe na bodaboda.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati