January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu chanjo ya uviko-19 yahimizwa

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Ili kufikia asilimia 100 ya watu kwa Mkoa wa Mwanza wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea,wawe wamepata chanjo ya uviko-19, waandishi wa habari wamehimizwa kuelimisha jamii ili kuweza kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma kupata chanjo hiyo.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa,ameeleza kuwa Mkoa huo hadi Oktoba 17, mwaka huu umeweza kuvuka lengo la kitaifa kwa kuchanja watu chanjo ya uviko-19 kwa asilimia 87.

Huku malengo ya serikali katika kuhakikisha kinga jamii inakuwepo dhidi ya uviko-19 ni kufikia asilimia 70 ya watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea ifikapo Desemba mwaka huu wawe wamepata chanjo ya uviko-19.

Dkt.Rutachunzibwa ameeleza hayo wakati akifungua kikao cha tathimini ya chanjo ya uviko-19 na uhuru wa habari wa kupata taarifa uliondaliwa na taasisi ya Internews kupitia mradi wa boresha habari na kuratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) kwa ufadhili wa shirika la USAID pamoja na Fhi360,ambacho kimeshirikisha waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza.

Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 Mkoa wa Mwanza ulikuwa na jumla ya watu milioni 1.8 wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea,ambapo tangu kuanza kwa zoezi la utoaji chanjo ya uviko-19 lililoanza Agousti,2021 hadi jana Oktoba 17,2022 Mkoa huo umeweza kuvuka lengo la kitaifa kwa kuchanja watu milioni 1.6 wenye umri huo.

Pia ameeleza kuwa kwa mujibu wa idadi hiyo ya sensa na ukilinganisha na watu waliochanjwa,takribani watu 200,000 wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea katika Mkoa wa Mwanza bado hawajapata chanjo ya uviko-19.

Aidha ameeleza kuwa udhibiti wa magonjwa ni kama vita, hivyo wanalazimika kutumia silaha mbali mbalimbali za kujikinga na magonjwa ili yasisambae kwenye jamii hivyo serikali pamoja na waandishi wa habari wana wajibu wa kuhakikisha jamii inapata uelewa ili kufikia lengo la kuwapata watu laki mbili ambao wamebaki kufikia lengo la kuchanja watu 1.8 milioni.

“Ili kufikia asilimia 100 ya watu mkoani hapa kuwa wamepata chanjo ya uviko-19 kwa kuhakikisha idadi ya watu 200,000, ambao hawajapata chanjo hiyo aidha wamepata dozi moja au hawakuchanja kabisa,waandishi wa habari mnajukumu la kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo hiyo,”ameeleza Dkt Rutachunzibwa.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho Mratibu wa elimu ya afya kutoka ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Renard Mlyakado, ameeleza kuwa kwa lengo la kitaifa Mkoa umefikia asilimia 87 ya uchanji chanjo hiyo kwa watu wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ikishika nafasi ya kwanza kwa kuchanja kimkoa ambapo asilimia 98.4 wamechanja chanjo hiyo huku ilioshika nafasi ya mwisho ni Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ambayo Ina asilimia 74.3.

“Mafanikio ya kuchanja idadi hiyo ni kutumia vyombo vya habari ikiwemo kutengeneza vipindi maalum vya kuhamasisha utoaji wa chanjo,ushirikishwaji wa viongozi wa serikali za mtaa,ambapo kwa pamoja kumesaidia wananchi kujitokeza kwenda kuchanja huku waliojitokeza zaidi ni wanawake wakiwemo wajawazito,”ameeleza Mlyakado.

Mlyakado, ameeleza kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), tangu kutokea kwa mlipuko wa uviko-19 duniani kwa Tanzania jumla ya visa 39, 679 vya uviko-19 vimeripotiwa huku vifo vikiwa 845.

Huku kwa idadi ya kidunia zaidi ya watu milioni 621.7 wameripotiwa kupata virusi na zaidi ya watu milioni 6.5 wakiripotiwa kufariki.

Aidha ameeleza kuwa kwa mujibu wa WHO katika kipindi hicho hadi sasa zaidi ya chanjo milioni 12.7,zimeshatolewa na kwa kipindi cha masaa 24 yaliyopita visa vipya 164, 921 vya maambukizi ya uviko-19 vimeripotiwa huku vifo vipya 274 vimetokea.

Awali Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko, ameeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kuwaelimisha waandishi waweze kuandika habari kwa weledi hususan habari za takwimu.

“Katika mafunzo haya waandishi 30 wataongezewa uelewa ili waweze kuripoti habari za Uviko-19 kwa ufasaha ambapo mada tatu zimewasilishwa ikiwemo ya namna bora ya kuandika habari za uviko-19 kiuweledi,nafasi ya chombo cha habari kwenye kuripoti habari za uviko-19 na uhuru wa habari,”ameeleza Soko.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa,akizungumza wakati akifungua kikao cha tathimini ya chanjo ya uviko-19 na uhuru wa kupata taarifa,ulioandaliwa na taasisi ya Internews na kuratibiwa na MPC kwa ufadhili wa shirika la USAID na fhi360.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko,akitoa neno la ufunguzi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa katika kikao cha tathimini ya uviko-19 na uhuru wa kupata taarifa uliondaliwa na taasisi ya Internews na kuratibiwa na MPC.kinachofanyika jijini Mwanza.
Baadhi ya washiriki wa kikao cha tathimini ya uviko-19 na uhuru wa kupata taarifa uliondaliwa na taasisi ya Internews na kuratibiwa na MPC.kinachofanyika jijini Mwanza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa,katikati walio Kaa huku wa pili kutoka kulia akiwa Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko,wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha tathimini ya chanjo ya uviko-19 na uhuru wa kupata taarifa,ulioandaliwa na taasisi ya Internews na kuratibiwa na MPC kwa ufadhili wa shirika la USAID na fhi360.