March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ELAF yatoa wito wa Umoja na maridhiano kwa watanzania

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

MKURUGENZI wa Taasisi ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF), Dkt. Khamis Masoud, ametoa wito kwa Watanzania kudumisha misingi ya amani, haki, uvumilivu na umoja katika kipindi hiki cha mpito wa kisiasa baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam mapema leo, Novemba 7, 2025 jijini Dar es Salaam, Dkt. Masoud alisema kuwa uchaguzi umepita, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kutumia busara, maridhiano na uvumilivu katika kujenga taifa lenye utulivu na mshikamano.

“Tunapojenga amani, tunapanda mizizi ya ustaarabu; tunapochochea hasira, tunavuna majivuno ya kihistoria. Huu ni muda wa busara na maridhiano, si wa lawama,” amesema Dkt. Masoud.

Amesema kuwa, jamii inapaswa kuponya majeraha ya kisiasa na maneno yaliyotokana na kampeni, kwa kuendeleza mazungumzo ya upendo, heshima na imani miongoni mwa wananchi.

Aidha, Dkt. Masoud ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, wa dini na wa kijamii kutumia lugha za maridhiano badala ya matamshi yenye kuibua mgawanyiko, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu Katiba na utu wa kila raia.

“Sheria inakuwa nuru inapolinda wote kwa usawa. Tunawasihi viongozi na wananchi wajiepushe na matamko yanayoweza kuibua hisia au kuchochea migawanyiko. Amani ndiyo urithi wetu wa pamoja,” ameongeza

Dkt. Masoud pia amewakumbusha vijana kujitenga na maandamano au vitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa taifa, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana tu pale ambapo amani inaimarika.

Aidha ameiomba serikali, viongozi wa dini na vyombo vya habari kuhimiza mazungumzo ya maridhiano na mshikamano wa kitaifa, huku akivitaka vyombo vya usalama kuhakikisha ulinzi wa raia wote bila upendeleo.