March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Duni: Othman ni Kiongozi wa kipekee, mzalendo asiye na Doa la ufisadi

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mkutano mkubwa wa kampeni za ACT Wazalendo umefanyika leo katika viwanja vya Gamba, Mkoa wa Kaskazini Unguja, na kujaza umati wa wananchi waliokusanyika kusikiliza sera na muelekeo wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika uwanjani hapo, Mzee Juma Duni Haji alimsifu kwa dhati Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, akimtaja kuwa ni kiongozi wa aina ya kipekee ambaye hajawahi kutokea katika historia ya Zanzibar.

Duni amesema, licha ya Othman kutumikia Serikali kwa muda mrefu katika nafasi nyeti serikalini, hajawahi kuhusishwa na tuhuma zozote za ufisadi au matumizi mabaya ya madaraka, jambo linalothibitisha uadilifu, uwazi, na dhamira yake ya kweli ya kulitumikia taifa kwa moyo wa kizalendo.

Amesema kuwa, tumemwona akihudumu katika nafasi mbalimbali za kitaifa bila kuchafuka. Huyu ni kiongozi safi, mwenye maono na anayeguswa na maisha ya wananchi wa kawaida.

Ameongeza kuwa huu ndio wakati wa Wazanzibari kusimama kwa umoja na kumpa Othman ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, ili kuleta mabadiliko ya kweli na kuijenga nchi yenye maendeleo, haki, na uwazi kwa wote.

Amesisitiza kwamba Zanzibar inahitaji kiongozi anayesimama na wananchi, na Othman ni mfano wa viongozi wanaochochea matumaini mapya kwa vizazi vijavyo.