October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dullah Mbabe, Twaha Kiduku wahesabu siku

Na Mwandishi Wetu

MABONDIA wanaofanya vizuri hapa nchini Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na Twaha Kassim ‘Kiduku’ sasa wanahesabu siku kuelekea kwenye pambano lao la ubingwa wa Taifa la taundi 12 uzito wa Super Middle litakalofanyika Agosti 28, katika uwanja wa Uhuru.

Mbali na kuwania ubingwa huo, pambano hilo pia litakuwa la kumaliza ubishi kati ya mambondia hao wawili ulidumu kwa muda mredu hata kabla ya kulishindwa kuumalizwa Oktoba 21 mwaka 2017 pale katika ukumbi wa Msasani ‘Msasani Club’ baada ya pambano lao kumalizika kwa sare.

Akizungumzia maandalizi yake kuelekea kwenye pambano hilo, Dulla ameuambia mtandao huu kuwa, toka amenza kujifua hadi sasa zikiwa zimebaki siku chache, anaamini kila kitu kimekamilika na anachokisubiri ni kumtoa nishai mpinzani wake ili kudhihirisha ubora wake.

Mbabe amesema kuwa, hana wasiwasi wowote na pambano hilo kwani kama alishindwa kumaliza ubishi miaka ya nyuma, sasa ni wakati wake kukamilisha hilo.

“Kwa upande wangu nimeshamaliza maandalizi hivyo nitahakikisha hiyo siku namkalisha mapema sana Kiduku ili kwanza kumaliza ubishi lakini pia kumtaka aache dharau kwani hata afanye nini ni lazima nitampiga kwenye pambano hilo, ” amesema Dulla Mbabe.

Katika mapamabo 27 ambayo Dulla Mbabe ameyacheza hadi sasa, ameshinda mapambano 24 yote kwa Knock Out huku akitoa sare katika mapambano matatu.

Akizungumzia pambano hilo, Kiduku amesema, maandalizi ya uhakika aliyoyafanya chini ya kocha wake Charles Mbwana ‘Power Ilanda’ yamemfanya azidi kujiamini na kujihakikishia ubingwa siku ya pambano.

Kiduku amesema kuwa, jambo linalompa uhakika kushinda pambano hilo ni kumchambua vema mpinzani wake na kuyasoma mapungufu yake hivyo watahakikisha anatumia udhaifu huo kushinda pambano hilo.

”Nilikuwa nasubiri kwa hamu kubwa pambano hili, hatimaye siku zinakaribia, namuomba Mungu azidi kutupa uhai, adhabu nitakayompa Dullah Mbabe hataisahau, nilikuwa namsaka muda mrefu sana hatimaye kaingia kwenye mtego wangu,” ametamba Kiduku.

Ata hivyo amewasisitizia mashabiki wa ngumi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo kwa ajili ya kushangilia ushindi wake sambamba na kupata burudani safi ulingoni.

Promota wa pambano hilo, Jay Msangi amesema, maandalizi yote kuelekea kwenye pambano hilo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 96 na kinachosubiriwa ni siku ya pambano lenyewe.

Hivi karibuni kiongozi huyo aliweka wazi kuwa, pambano hilo litasindikizwa na mabondia 12 watakaocheza pambano la utangulizi likiwemo moja la kick boxing.

Katika mapambano hayo, bondia Nasibu Ramadhan atapanda ulingozi kupimana nguvu na Ibrahim Class, Paul Kamata atapambana na Hussein Itaba, Halima Vunjabei atazichapa na Agnes Kayange, Rolen Japhet atapambana na Mastiki the Don huku Ramadhan Johncena atacheza na Habibu Pengo.