Na Is-haka Omar, Timesmajira online -Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapindizi(CCM)ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi,amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza atahakikisha vijana wanapewa ajira za kudumu ili wajikwamue kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa katika mkutano maalum wa kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Pangawe Wilaya ya Magharib ‘B’ Zanzibar.

Amesema endapo wananchi hao watamchagua kuwa Rais wa Zanzibar kwa awamu nyingine ataendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa vijana na makundi mbalimbali ya wananchi.
Dkt.Mwinyi,amesema kuwa ahadi zilizotolewa katika kampeni za mwaka 2020 zimetekelezwa kwa kiwango kikubwa ikiwemo miradi ya afya ,elimu ,miundombunu ya barabara, maji safi na salama na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Ambapo amesema endapo atachaguliwa katika awamu ijayo atatekeleza kwa kiwango kikubwa miradi mbalimbali ndani ya jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa skuli, ujenzi wa barabara pamoja na ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha mpira.
Kupitia hotuba yake Dk.Mwinyi, alihoji muenendo wa siasa za baadhi ya vyama vya upinzani na kueleza kuwa hawana sera wala ajenda za maendeleo kwani katika kampeni zao hawaelezi watafanya nini kwa wananchi mfano kutekeleza miradi ya elimu,kujenga barabara na hospitali badala yake wanatoa kauli za uchochezi.
Sambamba na hayo Dkt.Mwinyi,aliwaomba wananchi hao kumchagua kwa kura nyingi kuwa Rais wa Zanzibar,kumchagua Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wabunge,Wawakilishi na Madiwani wa CCM.
Naye Mgombea Uwakilishi Jimbo la Welezo kupitia CCM Hassan Khamis Hafidh,amesema kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Dkt.Mwinyi Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo yanayochewa na sera za chama hicho.
Hassan,ameeleza kuwa katika sekta ya afya Zanzibar imepiga hatua kubwa ambapo wananchi wanapata matibabu bure katika vituo vya afya na hospitali zenye vifaa tiba vya kisasa.
“Nawaombeni wananchi puuzeni kauli za baadhi ya wanasiasa wanaobeza maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya nane,kwani wameishiwa sera wanaanza kutafuta huruma ya wananchi kwa kupotosha wakati maendeleo yote yanaonekana kwa wazi,”amesema Hassan.

Aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis,amesema Zanzibar inanufaika na fedha za muungano zikiwemo za mfuko wa TASAF zinazowasaidia wananchi wote wa Unguja na Pemba.
Khamis,ameeleza kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakipotosha kuwa Zanzibar hainufaiki na fedha hizo jambo ambalo ni upotoshaji na kwamba wanatafuta umaarufu wa kisisasa na huruma ya wananchi.
Amesema katika historia ya Zanzibar Dkt.Mwinyi amevunja rekodi ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayogusa maisha ya wananchi wa rika mbalimbali.

.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako