March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Doyo aahidi kuwarudishia wananchi haki ya matumizi ya Pori la Rufiji kwa utaratibu Maalum

Na Mwandishi wetu,Rufiji, Pwani

Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiendelea na kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu, amefanya mkutano wa hadhara katika eneo la Muhoro, lililopo Jimbo la Rufiji, mkoani Pwani.

Katika hotuba yake, Doyo ameleza kusikitishwa na hali ya maisha ya wananchi wa Rufiji, licha ya jimbo hilo kuwa na bahati ya kuwa na mbunge ambaye amewahi kuteuliwa mara mbili tofauti kuwa waziri katika serikali.

Doyo ameswma ni jambo la kusikitisha kuona Rufiji bado haina barabara za uhakika, huduma za afya zikiwa duni, na katika baadhi ya maeneo hakuna zahanati kabisa, wakati jimbo hilo lina kiongozi mwenye dhamana kubwa serikalini. Alisisitiza kuwa wananchi wa Rufiji wanahitaji mabadiliko ya kweli, na kwamba hilo si kosa bali ni sehemu ya demokrasia. “Wananchi wa Rufiji wanahitaji mabadiliko ya kweli, na hilo si kosa, ni sehemu ya demokrasia,” amesema Doyo.

Doyo amesisitiza kuwa Chama cha NLD kimewaletea wananchi wa Rufiji mgombea ubunge Tatu Ally, ambaye ana dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo watu wa Rufiji. “Mabadiliko ya kweli yanahitaji ujasiri. Chagueni Tatu Ally kama mbunge wenu, na mimi kama rais wenu, tushirikiane kuleta heshima mpya kwa watu wa Rufiji,”ameongeza Doyo.

Aidha, Doyo alizungumzia changamoto za matumizi ya Pori la Akiba la Rufiji, akisema wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakinyanyasika kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa utaratibu mzuri wa matumizi ya rasilimali hiyo. Ameahidi kuwa serikali yake itahakikisha wananchi wa Rufiji wanaendelea kutumia pori hilo kwa vibali maalum, kwa manufaa ya kiuchumi bila kuharibu mazingira ya pori hilo. “Wananchi wa Rufiji wanastahili kupata huduma na fursa za kujipatia riziki kwa mujibu wa sheria, si kunyanyaswa katika pori hilo kama ilivyo sasa,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu, wakazi wengi wa Rufiji wanategemea uvuvi, kilimo, na utalii wa ikolojia, lakini miundombinu duni pamoja na ukosefu wa sera rafiki vimekuwa kikwazo kikubwa katika kuinua uchumi wa eneo hilo.

Doyo amewataka wananchi wa Rufiji kutumia fursa ya uchaguzi huu kufanya maamuzi yenye maslahi mapana kwao na kwa vizazi vijavyo. “Mabadiliko hayawezi kuletwa na mtu mmoja, bali na uamuzi wa pamoja wa wananchi,” amesema kwa msisitizo.

Kwa upande wake,Tatu Ally, mgombea ubunge wa Jimbo la Rufiji kupitia Chama cha NLD, amewataka wananchi kumpa ridhaa ili, kwa kushirikiana na Doyo, waongoze mageuzi ya kweli. “Kwa zaidi ya miaka 60, wananchi wa Rufiji wamekuwa wakisubiri maendeleo. Ni wakati wetu sasa wa kuandika historia mpya,” amesema Tatu Ally.

Msafara wa kampeni wa Chama cha NLD unaendelea kusonga mbele, huku ukielekea Kibiti, Dar es Salaam, na Morogoro, ukiwa na kaulimbiu ya “Uzalendo, Haki na Maendeleo.”