January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dodoma yajipanga kutatua changamoto za ajira kwa vijana

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI kwa Kushirikiana na Taasisi ya Strategius Advisory imeandaa Kongamano la siku mbili kuwakutanisha vijana waliohitimu Vyuo Vikuu na vya Kati wakiwemo waliofanikiwa kujiajiri na wasio na ajira.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Novemba 18,2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa kongamano hilo.

Senyamule amesema Kongamano hilo litafanyika Novemba 19 hadi 20,2024 ambapo litatoa fursa kwa wahitimu kujadili changamoto zinazowakwamisha na kujifunza kutoka kwa wenzao waliopata mafanikio katika kujiajiri au sekta binafsi.

“Jukwaa hili litasaidia wagitimu kujifunza mbinu mbalimbali za kujiajiri na kubuni fursa,huu ni mkakati wa kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana nchini,”amesema Senyamule.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Strategius Advisory,Lilian Mkumbo ametaja lengo la Kongamano hilo kuwa ni kuwawezesha vijana kwa kuwapa maarifa na uzoefu wa kujiajiri na kuendesha miradi ya kibiashara.

“Kongamano hili si la kuwatafutia vijana ajira bali linatoa maarifa kwa vijana kujua nini wafanye kujiajiri,

“Ambapo linatarajiwa kuwahamasisha vijana kuchukua hatua za kubadili maisha yao kwa kutumia ujuzi walioupata vyuoni na kujenga uwezo kwa kushindana katika soko la ajira na Ujasiriliamali,”amesema Mkumbo.