December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dodoma wataka ubingwa Taifa Cup

Na Nuru Mkupa, TimesMajira Online, Dodoma

CHAMA cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dodoma ambao wamepewa uwenyeji wa michuano ya mchezo wa Kikapu ya Taifa Cup ambayo itaanza kutimua vumbi kuanzia Novemba 11 hadi 21 kwenye viwanja vipya vya Chinangari maarufu kama Jakana Pack, wamepania kubakiza ubingwa wa michuano hiyo.

Tayari wameshaanza maandalizi kuelekea katika mashindano hayo na wamejipanga vizuri katika kila idara ili kuhakikisha ubingwa unasalia Mkoani hapa.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Mkwama (Big Beny) ameliambia Majira kuwa, Mkoa wa Dodoma utawakilishwa na timu tano ambazo kati ya hizo za wanaume ni tatu na mbili za wanawake na tayari wachezaji wa timu hizo wameshapatikana kupitia uteuzi uliofanywa kwenye Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dodoma iliyomalizika jijini hapa.

Amesema, ili kufanya vizuri na kutimiza malengo yao ya kubakiza ubingwa katika michuano hiyo, ni lazima timu hizo kufanya mazoezi ya kimkakati uku akiwakumbusha viongozi wa timu hizo kutimiza wajibu wao wa kuwahimiza wachezaji kuhudhuria mazoezi .

“Ligi hii tunaifanyia nyumbani kwetu hivyo tunayo nafasi kubwa sana ya kufanya vizuri Kwa kuzingatia kuwa tutakuwa na mashabiki wengi wa nyumbani, hali ya hewa tumeizoea lakini pia timu zetu zinaendelea na maandalizi ya mazoezi ya kimkakati hivyo niwaombe wanamichezo wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kujionea vipaji vya mchezo huo na kupata burudani, ” amesema Beny.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya maandalizi ya Taifa Cup, Derrick Mafuru amesema kuwa, hadi sasa maandalizi yote yanaenda sawa ikiwa ni pamoja na kuratibu timu shiriki pamoja na upatikanaji wa huduma zote muhimu.

Japokuwa mambo yote yanakwenda sawa lakini bado kuna changamoto ya timu shiriki kuchelewa kuthibitisha ushiriki wao jambo linalokwamisha baadhi ya mambo humuhi na kuwataka viongozi wa timu hizo kuthibitisha ushiriki wao ili kutoka fursa ya mambo mengine yaendelee.

Katika hatua nyingine, timu ya Don Bosco Panther imefanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi ya kikapu Mkoani humo baada ya kuifunga Dom Spurs kwa pointi 74-54 katika mchezo wa pili wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Vijana Wajenzi jijini hapa.

Licha ya fainali hiyo kupangwa kuchezwa mechi tatu lakini ilikamilika kwa michezo miwili ambayo yote timu ya Don Bosco ilifanikiwa kuibuka na ushindi ambapo kwa mujibu wa kanuni hata kama Dom Spurs ingeshinda mchezo mmoja uliobaki bado usingekua na maana yoyote kwa kutwaa ubingwa huo.