March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia:Nikishinda nitaongeza misaada kwa jamii

Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo jipya la Uyole kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Tulia Ackson, amesema endapo atachaguliwa ataendelea kuongeza misaada kwa jamii sambamba na kuviwezesha vikundi mbalimbali vya kijamii ili kukuza uchumi wa wananchi.

Amesema vikundi hivyo vitajumuisha mama lishe, makundi ya wazee, maafisa usafirishaji, watu wenye ulemavu pamoja na makundi mengine yenye uhitaji, huku akiahidi kuanzisha shughuli za kijamii zitakazochangia maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza Septemba 13, 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni zake katika Uwanja wa Shule ya Msingi Hasanga, Uyole, Dkt. Tulia pia amewaomba wananchi kuwachagua madiwani wote wa CCM ili utekelezaji wa ilani uwe rahisi na kwa ufanisi.

Aidha, amesema anakusudia kuunganisha vikundi vya kijamii vinavyohusiana na masuala ya kufa na kuzikana na taasisi za kifedha pamoja na wadau wa maendeleo, ili vikundi hivyo visiishie kwenye shughuli za mazishi pekee bali viweze kujikwamua kiuchumi.

“Nitajitahidi nikichaguliwa kuwa Mbunge wa Uyole kusaidia vikundi vingi ikiwemo vya bajaji, mama lishe, watu wenye ulemavu, makundi ya vijana na wazee ili kuviinua kiuchumi,” amesema.

Katika sekta ya michezo, Dkt. Tulia amesema atashirikiana na wadau mbalimbali kuinua vipaji vya vijana kupitia michezo yenye tija kiuchumi, akisisitiza mchezo wa ngumi kama miongoni mwa michezo inayoweza kuwakwamua vijana wa Uyole.

Kuhusu makazi bora, amebainisha kuwa atashirikiana na madiwani, wenyeviti na mabalozi wa mashina kuwabaini wananchi wanaoishi katika mazingira magumu na kuwasaidia kujengewa nyumba bora.

Vilevile, Dkt. Tulia amesema ataangalia namna ya kusaidia vikundi vilivyopo ndani ya taasisi za kidini ili viweze kustawi na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii.

Amesisitiza kuwa moja ya kazi zake za awali akichaguliwa ni kufanikisha uanzishwaji wa Halmashauri ya Uyole, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi litakalowezesha kusukuma kasi ya maendeleo ya jimbo hilo jipya.

Sambamba na hilo, amesema atahakikisha miundombinu ya barabara inaboreshwa, ikiwemo barabara za mitaa kujengwa kwa kiwango cha lami, vivuko na madaraja kwenye kata zote pamoja na kukamilisha barabara ya njia nne kutoka Uyole hadi Ifisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Hamfrey Nsomba, amesema Dkt. Tulia amekuwa mbunge wa mfano kwa kipindi chote alichohudumia Jimbo la Mbeya Mjini kabla ya kugawanywa, kwani alifanikiwa kuleta miradi mingi kupitia ushawishi wake kwa serikali.

Naye mmoja wa wananchi wa Uyole, Watson Kihaga, amesema wanamatumaini makubwa kuwa Dkt. Tulia ataendelea kushughulikia changamoto za jimbo hilo zikiwemo barabara, maji na huduma nyingine muhimu.