November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

RAIS wa Mabunge Duniani  na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson ameshiriki ibada Kanisa la Baptist Isyesye Madhabahu ya Sauti ya Rehema na sauti ya uponyajiKata ya Isyesye huduma inayoongozwa na Mchungaji Patrick Mwalusamba .

Aidha Dkt.Tulia amewataka
Waumini kuendelea kuombea amani nchini huku akiwasisitiza kushiriki uchaguzi utakaofanyika novemba 27 mwaka huu.

Dkt.Tulia amesema Waumini wanawajibu wa kwenda kusikiliza kampeni za uchaguzi ili wapate viongozi watakaowaletea maendeleo katika mitaa yao.

Aidha ameipongeza huduma hiyo kwa namna inavyozidi kukua siku hadi siku.

Dkt.Tulia Ackson amesema Waumini wasiposhiriki kupiga kura wasiwe na sababu za kuwalaumu viongozi watakaochaguliwa kwa kuwa wao wameshindwa kuitumia fursa hiyo.

Amehitimisha kwa kuwashukuru Waumini kwa kumuombea Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na viongozi wote akiwemo yeye ndiyo maana amani inaendelea kuwepo nchini.

Awali Mchungaji Patrick Mwalusamba amempongeza Dkt.Tulia kwa kufika ibadani licha ya majukumu mazito ya Jimbo,Taifa na Dunia.

Mwalusamba amesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu uwe huru na haki ili nchi ipate viongozi watakaodumisha amani na kuwaletea maendeleo wananchi.

Mwalusamba amewahimiza Waumini wasikose kushiriki kupiga kura kwani hata biblia inasisitiza masuala ya uchaguzi.

Naye Victor Baraka muumini wa huduma hiyo amesema binafsi ujio wa Dkt.Tulia  umempa faraja kwani ni viongozi wachache wenye moyo kama wake na amehimiza wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa bila kujali itikadi zao.

Watanzania wanatarajia kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa novemba 27,2024 utakaowaweka madarakani viongozi wa vitongoji, vijiji na Mitaa uongozi utakaodumu kwa kipindi cha miaka mitano.