November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia akabidhi tofali 9000 Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya

Na Esther Macha, Timesmajira Online,Mbeya

SPIKA wa Bunge,Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ,Dkt Tulia Ackson amekabidhi tofali 9000 zenye thamani ya shilingi mil.24 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya upasuaji wa moyo, mishipa ya fahamu pamoja na kichwa kwa hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa hivi karibuni kuunga mkono juhudi za hospitali na wadau.

Akizungumza leo wakati wa kukabidhi tofali hizo kwa uongozi wa hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya,Dkt.Tulia amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa vyumba hivyo kutasaidia kupunguza umbali mrefu wa kufuata huduma jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nje ya nchi.

Amesema kuwa huduma hiyo pia itasaidia wananchi wanaoizunguka nchi pamoja na kuleta fedha za kigeni sababu huduma hizo watakuwa hawapati bure kama wananchi wale ambao hawajiwezi.

“Tunaamini kwamba juhudi mbalimbali zinazofanywa zinaunga mkono mpango mzima wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa ni kitovu cha mambo mengi ikiwemo huduma ya afya,”amesema Dkt.Tulia.

Dkt.Tulia amesema kuwa pamoja na huduma za afya nzuri wanazotoa na changamoto nyingine wanajitahidi kuwa wabunifu ili kuweza kutoa huduma iliyo kamilika.

Aidha amesema kuwa alitoa ahadi ya matofali 9000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba hivyo vitatu ambayo ameitekeleza hivyo ameomba wadau waendelee kujitokeza kuchangia ili vyumba hivyo viweze kukamilika na huduma zote ziweze kutolewa.

Mkurugenzi hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt.Godlove Mbwanji amesema kuwa Mbeya ipo kimkakati katika mpango wa taifa wa kuongeza tiba utalii kwa nchi zinazotuzunguka kuja kupata matibabu kwani miaka mingi wananchi walikuwa wakipelekwa India,Afrika kusini na kutumia fedha nyingi.

“Hivi juzi nimetoka Dodoma katika kupanga mikakati ya kuendelea kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika sekta ya afya ili wananchi wawe na uhakika wa kupata matibabu na wasiende nje ya nchi,pia tuweze kuvutia wananchi wa nchi zinazotuzunguka badala ya wao kwenda India waje Tanzania, imeonekana Mbeya ipo eneo ambalo ni la kimkakati Kuna watu wengi wanaohitaji huduma,”amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi, Daktari Bingwa wa masuala ya upasuaji Dino Mwaja amesema majengo hayo yatakamilika kwa wakati na wagonjwa wataanza kupatiwa huduma Ili kuokoa maisha yao.