January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Tulia aiomba Benki ya NMB kuendelea kusaidia madawati Mbeya

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

SPIKA wa Bunge na mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt.Tulia Ackson ameiomba benki ya NMB kuiangalia Mbeya kwa jicho la pekee katika suala zima la madawati kwa shule za msingi na sekondari kutokana na kukabiliwa na uhaba wa madawati unaopelekea watoto kukaa chini madarasani.

Dkt. Tulia amesema hayo jana wakati akipokea msaada wa madawati 100 kwa shule ya sekondari ya Iduda iliyopo mkoani hapa kutoka benki ya NMB.

Hata hivyo Dkt. Tulia amesema kuwa benki ya NMB waiangalie Mbeya Mjini kwa kwa jicho la upekee wanavyopita kwa wadau.

“Hapa Mbeya Mjini pamoja na msaada huu leo wa madawati ambao ulikuwa ombi maalum, lakini bado tuna changamoto ya watoto wetu kukaa chini na sisi kama Halmashauri tumeazimia watoto wetu wa shule za msingi na sekondari hakuna kukaa chini hivyo tunaamini kuwa hawa ndugu zetu wa benki ya NMB wanao uwezo wa Muungano na sisi ili watoto wasikae chini”amesema Spika Dkt. Tulia.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu wateja binafsi na biashara wa Benki ya Nmb, Filbert Mponzi amesema Kuwa akikabidhi 100 kwa shule ya sekondari Iduda yenye kidato cha tano na sita.

Mponzi amesema kuwa bado benki hiyo itaendelea kusapoti masuala ya elimu na afya na kwamba kwa kishirikina na wizara ya elimu wamekuwa wakifika katika shule mbali mbali kutoa elimu ya kifedha.

“Bado tutaendelea kuiangalia upande wa elimu na afya kutokana na umuhimu wake katika jamii kikubwa walengwa wanapoomba ni kufuata taratabu tu” amesema Mponzi.

Diwani wa kata ya Iduda, Pishoni Taraban amesema kuwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa na serikali wananchi nao wameweza kujitolea kujenga madarasa 10 na ofisi tano za walimu kwa shule za msingi Mwala na Iduda.