March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Serera: Ubora wa Huduma kwa Wateja ni Kigezo Kikuu cha Ushindani wa Kibiashara

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Hassan Serera, amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo la utoaji wa huduma, hasa kutokana na ongezeko la watanzania wanaoshiriki moja kwa moja katika uwekezaji na utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo za Wiki ya kimataifa ya Huduma kwa Wateja Tanzania 2025 iliyoandaliwa na Taasisi ya CSW, Dkt. Serera alisema maendeleo hayo yanaonesha namna ambavyo nchi imeendelea kuwaandaa wananchi wake kushiriki kikamilifu katika sekta ya huduma na biashara.

“Kama nchi tunajipima vizuri katika suala la utoaji wa huduma kwa sababu kipimo cha kwanza ni aina ya watu wanaohusika katika uwekezaji. Wanaotoa huduma nyingi sasa ni Watanzania wazawa, jambo linaloonesha tumepiga hatua kubwa katika kuwaandaa watu wetu,” alisema Dkt. Serera.

Aliongeza kuwa ili kuvutia wawekezaji wa nje, ni muhimu kuwa na wananchi walioboreshwa kitaaluma na kiutendaji katika sekta ya huduma. Amesema katika hafla hiyo ya tuzo, imeonekana wazi kuwa watanzania wengi sasa ndio wanaosimamia huduma, kukutana na wateja, na kuendesha shughuli kwa ufanisi mkubwa.

“Tumeona watu waliopokea tuzo na walioongozana nao ni Watanzania. Hawa ndio wanaokutana na wateja wetu wa ndani, wanazungumza lugha ya ushawishi na kutoa huduma bora. Huu ndio ushindani tunaoutaka kuona katika taasisi na makampuni yetu,” alisisitiza.

Aidha, Dkt. Serera alitahadharisha kuwa taasisi au kampuni yoyote isiyotoa huduma bora inahatarisha kupoteza wateja wake, akisema, “Mteja akihudumiwa vibaya, ni rahisi asirudi tena. Hivyo, huduma bora ni msingi wa biashara endelevu.”

Akizungumzia hali ya ushindani wa kibiashara, alisema biashara na uzalishaji sasa vinahitaji ubunifu na ubora wa huduma kama silaha kuu ya ushindani. Alisisitiza kuwa hata nchi zilizoendelea zimewekeza zaidi katika kuboresha huduma kwa wateja, na Tanzania haipo nyuma, kwani taasisi nyingi zimeendelea kuboresha mifumo yao ya huduma.

“Mtanzania kwa asili ni mkarimu, lakini sasa tunapaswa kuongeza ubora katika huduma zetu. Bidhaa bora bila huduma bora bado haijakamilika,” alisema Dkt. Serera.

Aidha, alimpongeza taasisi ya CSW kwa kuandaa hafla hiyo ambayo ilihusisha utoaji wa zaidi ya tuzo 20 kwa taasisi na kampuni zilizoonyesha ubora wa huduma katika Wiki ya Huduma kwa Wateja.

“Nawapongeza waliopata tuzo na wale walioandaa. Hii ni njia ya kuthibitisha kuwa juhudi zao zinafuatiliwa kwa karibu, na zinachangia katika kuinua viwango vya huduma nchini,” alisema Dkt. Serera.

Kadhalila, Dkt. Serera alihimiza taasisi zote, hususan za serikali, kuendelea kuboresha huduma zao, akisema hata wale ambao hawajapata tuzo mwaka huu wamepata fursa ya kujifunza na kuboresha zaidi huduma wanazozitoa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Uyo anelise ni Annelise Nyangusi, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa CSW Group, amesema kuwa katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, huduma kwa wateja ni chachu muhimu ya kukuza biashara na kampuni hivyo kama CSW Tanzania, wameona umuhimu wa kutambua na kutunuku kampuni, mashirika na wafanyabiashara wanaofanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa wateja, kwa kuzingatia vigezo maalum vinavyoonyesha ubora wa utendaji wao.

Amefafanua kuwa mchakato wa kutambua washindi hao unaanza ndani ya kampuni kupitia kamati maalum inayofanya utafiti kwa kutumia vigezo mbalimbali ili kubaini kampuni zinazostahili pongezi kwa ubora wa huduma zao kwa wateja.

Naye Irene Gowele, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), aliwashukuru waandaaji wa tuzo hizo akibainisha kuwa TANESCO inajivunia kupokea tuzo hiyo kwa kuwa ni miongoni mwa mashirika ya umma yanayofanya vizuri katika eneo la huduma kwa wateja.

Amesema mafanikio hayo ni matunda ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya nishati.

“Hii inakwenda kutuongezea ari na chachu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi, kuhakikisha tunawahudumia wateja wetu kwa wakati na kuwasiliana nao kwa ufanisi,” alisema Gowele.

Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya nishati umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma kwa wateja, jambo lililowezesha shirika kufikia hatua ya kushinda tuzo hiyo.

Ametoa pongezi kwa Serikali, Wizara ya Nishati, Bodi ya Wakurugenzi na wafanyakazi wote wa TANESCO kwa ushirikiano wao, akisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa kuboresha huduma kwa wateja.

Gowele ameongeza kuwa shirika limeendelea kufanya maboresho mbalimbali katika eneo la huduma kwa wateja, ikiwemo ununuzi wa vitendea kazi kama pikipiki, bajaji na magari, ili kuhakikisha wateja wanahudumiwa kwa wakati katika maeneo yote nchini.

Steven Mkomwa Mkurugenzi Mkuu
Chemba ya Sekta ya Ujenzi na Miundombinu ya Tanzania (CCIT) alisema kuwa tuzo hiyo ni uthibitisho wa kutambuliwa kwa mchango wa taasisi yao katika utoaji wa huduma bora kwa wateja ndani ya sekta ya miundombinu na ujenzi.

Aidha, aliongeza kuwa tuzo hiyo imekuwa chachu ya kuendeleza kuboresha huduma na kuleta ubunifu zaidi katika sekta ya ujenzi nchini.

Philemon Matoi, Mkurugenzi wa Masoko na Usambazaji wa kampuni ya LS General Supply Ltd, ambao wamebobea katika uingizaji na usambazaji wa taulo za kike na ni wadhamini wakuu wa hafla hiyo, alisema kuwa wanafurahi kuwa miongoni mwa washiriki na washindi wa tuzo hizo.

Aliongeza kuwa wanaamini tuzo hizo zinachochea uhusiano mzuri kati ya biashara na biashara, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha tuzo hizo zinaendelea kuwa endelevu kwa manufaa ya sekta nzima ya biashara nchini.
Ayubu Mbarazi, Meneja wa Masoko na Burudani kutoka Amell, alisema tuzo waliyoipata katika kipengele cha Mgahawa Bora (Best Restaurant) ni matokeo ya jitihada na ubora wa kazi zao.

Aliongeza kuwa watendelea kuongeza juhudi zaidi katika kutoa huduma bora kwa wateja wao ili kuhakikisha kampuni inaendelea kukua na kutoa huduma zenye viwango vya juu zaidi.