November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia:ujenzi wa miundombinu itumike kufungua nchini kiuchumi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,amesema ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini inayoendelea siyo mapambo bali itumike kufungua uchumi wa Tanzania.

Dkt.Samia amesema hayo Juni 14,2023 mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa meli mpya ya Mv.Mwanza Hapa Kazi tu,katika Bandari ya Mwanza Kusini ikiwa ni siku yake ya tatu ya ziara mkoani hapa.

Ambapo amesema kuwa itatumika kwa watanzania kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha viwandani na shambani ili bidhaa zao zisafirishwe kwa kutumia miundombinu hiyo kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi na hilo ndilo jambo la pili na kubwa.

“Hii ndio maana ya tunakwenda kufungua Tanzania kiuchumi,sasa tunajenga meli,madaraja,bandari,reli, barabara haya yote siyo mapambo bali yatumike kufungua uchumi wetu wa Tanzania hii ina maana kwamba kuwepo kwa miundombinu ni jambo moja lakini kwa sisi watanzania kufanya kazi kwa bidii,tuzalishe shambani na viwandani ili bidhaa zetu zisafirishwe tukauze nje ya nchi na ndio jambo la pili na kubwa,”amesema Dkt.Samia.

Amesema miundombinu hiyo inakwenda kupeleka sokoni kila kinachozalishwa nchini na kazi hiyo haijafanywa Mwanza pekee inafanyika Kigoma ili waende kwenye soko la DRC Congo.

“Kazi hii inafanyika Mwanza,bandari ya Tanga ili kusafirishwa nchi jirani,pia inafanyika Dar-es-Salaam na kule Zanzibar ili nchi ya Tanzania ifunguke,tuzalishe,tuuze,tusafirishe wa ndani waende nje na wa nje waje ndani ili uchumi wa Tanzania ufunguke,”amesema Dkt.Samai.

Huku akisisitiza kuwa wakati serikali ikishughulika na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini wananchi waendelee na kazi ya uzalishaji.

Sanjari na hayo amesema katika bandari ya Mwanza Kusini mbali na ujenzi wa meli mpya ya Mv.Mwanza hapa kazi tu pia kuna meli nyingine ambayo itakuwa inabeba mabehewa na kuyasafirisha nje ya nchi.

“Treni ikifika hapo itashusha moja kwa moja mabehewa kama yalivyo na kubebwa katika meli hiyo ambayo serikali imeikarabati kwa mamilioni kadhaa itabeba na kupeleka katika bandari nyingine zaidi za nje ya nchi yetu na itakuza biashara,”amesema Dkt.Samia na kuongeza kuwa

“Meli ya Mv.Mwanza hapa kazi tu tumejenga kwa zaidi ya milioni 100, na kazi ndani ya meli inakwenda vizuri na itabeba watu zaidi ya 1000 na tani 400 za mizigo,baada ya miezi miwili tutakabidhiwa na nitakuja kuzindua,”amesema Dkt.Samia.

Awali Dkt.Samia akizungumza na wananchi wa Misungwi na Sengerema mara baada ya kukagua ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi (JPM),amewataka wananchi hususani wanaofanya kazi katika mradi huo kutoa ushirikiano na kuacha kuiba vifaa.

Ambapo amewashukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika ujenzi wa daraja hilo na litakapo kamilika ni faida kwa watanzania wote na faida kubwa zaidi ni kwa wakazi ambao wapo jirani na daraja hilo ambalo limeanza kutoa ajira kwao na litaendelea kutoa ajira maisha yake kwa sababu sasa ni kituo kikubwa cha magari yanayopita kwenda nje ya nchi na sehemu mbalimbali za nchini hapa.

Rais huyo amesema kuwa daraja hilo ujenzi wake up asilimia 70 na kazi ni nzuri ya ujenzi, wanategemea litakuwa daraja madhubuti na Matumaini yao linakwenda kukamilika kwa wakati na watakabidhiwa kwa wakati.

“Niwaombe sana mtoe ushirikiano wale wenye mikono midogomdogo hasa mnaofanya kazi mara kipande cha nondo,mara saruji,mara nini hapana,hili daraja ni letu tusiharibu daraja letu kwaio niombe sana ushirikiano,kwani mmetoa ushirikiano mpaka sasa hivi daraja limefikia asilimia zaidi ya 70, tunaamini litakamilika kwaio tuwaache wakandarasi wafanye kazi yao vizuri ili kujenga daraja madhubuti,”.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa daraja hilo lina urefu wa kilomita 3 pamoja na barabara unaganishi yenye urefu wa kilomita 1.66 ambalo litagharimu takribani bilioni 716.

Prof.Mbarawa amesema hakuna kitu chochote kilichosimama mradi unaendelea kutekelezwa Masaa 24 kwa siku na wataalamu wamejipanga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

“Tutaendelea kusimamia daraja hili na kuhakikisha kila kazi inayofanyika inafanyika kwa viwango vinavyokubalika na mkataba kama daraja hili maisha yake ni kuishi kwa miaka 200 litaishi kwa miaka 250,”amesema Prof.Mbarawa.