March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia:Tumedhamiria kutegua kitendawili cha upatikanaji wa maji Mwanza

*Azindua mradi chanzo kipya cha maji Butimba, kunufaisha wananchi 450,000

*Awataka wananchi kulipa ankra za maji

*Aonya ubambikaji wa ankra za maji kwa wananchi

*Asisitiza utunzaji wa mazingira na Ziwa Victoria 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza 

Serikali imesema imedhamiria  kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji mkoani Mwanza yenye kutosheleza wananchi huku wito ukitolewa kwa  wananchi kulipa ankra za maji ili huduma iwe endelevu.

Hayo yamebainishwa  Juni 20,2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,mara baada ya kuzindua mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba, wilayani Nyamagana jijini Mwanza ambacho kimegharimu kiasi cha bilioni 71 na kina uwezo wa kuzalisha lita za  ujazo milioni 48 kwa siku.

Mradi huo umetekelezwa na Serikali kwa ufadhili wa mkopo nafuu kutoka kwa wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya Uwekezaji ya Ulaya  na Shirika la Maendeleo la Ufaransa pamoja na Umoja wa Nchi za Ulaya chini ya programu ya maji safi na usafi wa mazingira Ziwa Victoria.

“Mradi huu ulisubiriwa kwa muda mrefu,nakumbuka katika  ziara zangu Mkoa wa Mwanza mara  mbili  nilielekea eneo hili na kilio kikubwa cha  wananchi kilikuwa ni maji,niliwaambia subirini maji yatakuja Butimba na leo mmepata maji safi na salama.Mimi na wenzangu serikalini,tumedhamiria kuhakikisha tunategua kitendawili cha upatikanaji wa maji safi na salama yenye kujitosheleza kwa  wananchi  wote wa Jiji la Mwanza na viunga vyake,”.

Dkt.Samia,amesema,chanzo cha maji Butimba,kitaboresha hali ya huduma ya  upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi takribani 450,000, wa Jiji la Mwanza na viunga vyake.Huku akitaka mradi huo ulindwe na uwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho kwani uwekezaji  wake umegharimu fedha nyingi.

“Miradi mingine inayotekelezwa chini ya programu hiyo ni ujenzi wa matenki  ya maji maeneo ya miinuko katika Jiji la Mwanza,kwa miaka ya nyuma hatukudhania Mwanza kule juu ya milima kutakuwa na matenki ya maji,pia tumefanya ujenzi wa mfumo wa uondoaji maji taka maeneo mbalimbali ikiwemo milimani,pia katika  gereza la Butimba,”amesema Dkt.Samia na kuongeza:

“Miradi hiyo imelenga kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira,ikiwa ni pamoja na kulinda mazingira ya Ziwa Victoria,ambalo ni muhimu kwa maisha ya wakazi wa Jiji la Mwanza na wanaoishi Kanda ya Ziwa hilo na maeneo ya jirani.Nimefurahi kusikia mradi huu pia ulihusisha ujenzi wa vyoo vya kisasa 107 kwenye maeneo ya umma ikiwemo shuleni,sokoni na stendi kwa Wilaya ya Nyamagana na Ilemela,”.

“Juhudi za kuhifadhi mazingira ziendelee kufanyika kikamilifu kwa kushirikiana na taasisi zote.Huu ni mradi mkubwa lazima tutunze mazingira ili ziwa liendelee kuwepo na liwepo kwa vigezo vyake lisikauke tukarudi tena huko nyuma.Mindombinu na uwekezaji tuliofanya ni wa thamani, wagharama kubwa  kwaio  wote tushirikiane kulinda mazingira ili ziwa liwe chanzo cha uhakika cha upatikanaji wa maji ndani ya Kanda hii ya ziwa,”.

Sanjari na hayo amewataka wananchi kulipa ankara za maji ili zitumike kuendesha miundombinu na kutoa huduma iwe endelevu, huku akiwaonya watumishi wa idara ya maji kutowabambikizia wananchi ankara za  huduma ya maji.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, amesema kwa sasa mahitaji ya maji kwa Mkoa wa Mwanza ni lita za uzajo  milioni 172 kwa siku, lakini kwa sasa uzalishaji ni lita za ujazo milioni 138, kutoka vyanzo viwili vya maji ambavyo ni Capripoint na cha Butimba ambacho Rais amekizundua.

Hivyo mradi huo umesaidia kupunguza changamoto ya hupatikani wa maji  kwa kiasi kikubwa jijini Mwanza,Huduma ya maji  kwa Mkoa wa Mwanza inatolewa na taasisi tatu ikiwemo Mamlaka  ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) hapa mjini,SEWASA  wilayani Sengerema na RUWASA kwa upande wa vijijini.

Ambapo amesema,kwa mwaka 2021 wakati Rais Samia anaingia madarakani hali ya upatikanaji wa maji mjini kwa Mkoa wa Mwanza ilikuwa asilimia 57 lakini hadi kufikia mwaka 2025 umefikia asilimia 85 sawa na ongezeko la asilimia 27.Na  Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza zimeonesha  ongezeko la upatikanaji wa maji,ambapo kwa Wilaya ya Misungwi imeongeza huduma kutoka asilimia 12 na kufikia asilimia 90.

Huku Wilaya ya Magu kutoka asilimia 55 hadi asilimia 93.3, Sengerema wamefikia asilimia 92 kutoka asilimia 61, Ilemela kutoka asilimia 80 hadi asilimia 90, Nyamagana kiwango kimeongezeka kutoka asilimia 59 hadi asilimia 78, Ukerewe kutoka asilimia 69 hadi kufikia 81 na Wilaya ya Kwimba kutoka asilimia 67 hadi 78.

Amesema miradi inayoendelea kutekelezwa Wilaya ya Nyamagana ni pamoja na mradi wa maji katika maeneo ya Buhongwa,Kishiri,Kisesa,Usagara na maeneo jirani,ambapo kiasi cha bilioni 46.2,zimeisha wekwa na mpaka sasa miradi hiyo imefikia asilimia 76 ya utekelezaji wake.

Pia kuna mradi wa kuboresha huduma ya hupatikanaji wa maji maeneo ya Luchelele  bilioni 4,ambapo umefikia asilimia 85 ya utekelezaji wake.Huku hali ya upatikanaji wa maji vijijini kwa  Mkoa wa Mwanza imeongezeka kutoka asilimia 57 mwaka 2021 hadi asilimia 77  mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 20.

Katika kipindi cha mwaka 2021/2025 hali ya upatikanaji maji vijijini imeimarika kwa kiwango kikubwa  kwa Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza na wastani wa hupatikanaji wa maji vijijini imeongezeka kutoka asilimia 57 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 81.

Kuanzia Machi 2021/2025,Mkoa umekamilisha jula miradi  80 kwa upande wa maji vijijini yenye thamani ya bilioni 100.3,kupitia Mamlaka ya Maji Vijijini(RUWASA).

Kwa upande wake Waziri wa Maji,Jumaa Aweso,amesema,anakiri kuwa ulikuwa ni mtihani,wananchi walikuwa wanahoji kwanini maji yaende mikoa mingine ili hali walio karibu na ziwa wanapata changamoto ya maji.

“Nimekaa katika Wizara ya Maji kwa miaka 8, dhana ya maji ilikuwa  kero na lawama,asilimia kubwa wanaoteseka na adha ya maji ni wakinamama na Rais hakutaka kusikia wala kuona wanateseka kwa ajili ya adha ya maji,ile miradi 177,ambayo ilikuwa haitoi maji sasa inatoa,”.

Aweso,amesema vijiji 12,318  vilikuwa havina maji hapo awali lakini kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia tayari vijiji 10576 vimepata maji huku vikisalia takribani vijiji 1500.