November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia:Serikali yachukua hatua kukabiliana na uhaba wa chakula,mfumuko wa bei

Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha inakabiliana na upungufu wa chakula pamoja na mfumuko wa bei ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa skimu kwa ajili ya umwagiliaji ili kama nchi iwe na msimu miwili ya mavuno.

“Tumetenga fedha nyingi sana kwa ajili ya kujenga skimu za umwagiliaji hii maana yake nini,wakulima tulime mara mbili kwa mwaka tuvune mara mbili kwa mwaka badala ya kutegemea mvua ambayo inatufanya tuvune mara moja kwa mwaka, amesema Dkt.Samia na kuongeza kuwa

“Hatua nyingine nikutoa mbolea kwa ruzuku tulianza mwaka jana changamoto zikajiyokeza mwaka huu vyama vya ushirika ndio vitasambaza na wanategemea itawafikia kila mwananchi ambaye ni mkulima,”.

Dkt.Samia ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa tamasha la Bulabo linalofanyika Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza ambapo ikiwa ni moja ya ziara yake ya siku nne mkoani hapa ambapo amesema kuwa ulimwengu mzima sasa unatarajia kuwa na upungufu wa chakula pamoja na mfumuko wa bei.

Ameeleza kuwa sababu ya mfumuko na upungufu wa chakula ni kutokana na athari za Uviko-19,vita inayoendelea huko Ulaya na kubwa zaidi ni mabadiliko ya tabianchi.

“Sababu hizi tatu kwa kipindi cha miaka mitatu,minne mfululizo hivi sasa zimefanya nchi zetu haziwezi kuzalisha chakula cha kutosha na kule kwenye chakula cha kutosha kuna vita na vikwazo vimewekwa kiasi ambacho chakula hakiwezi kutoka kwenda maeneo mengine kwa maana hiyo ulimwengu unatarajia kuwa na upungufu wa chakula na unaleta mfumuko wa bei na matarajio ya ulimwengu mwaka huu mfumuko wa bei ni asilimia tano lakini kilichotokea sasa mfumuko wa bei unaanzia kwenye asilimia 10 kwenda mbele, na hii ni kwa mabara yote,”amesema Dkt.Samia.

Nchi mbalimbali zinachukua hatua kurekebisha ili wananchi wasiumie na mfumuko huo wa bei ambapo Tanzania pia imefanya hivyo hivyo ambapo waliopata mfumuko wa bei katika mafuta na mbolea waliweka ruzuku na bei ikashuka ambapo mpaka sasa nchi imeendelea kuzuia mfumuko huo wa bei kwenye chakula.

Pia amesema,sababu hizo tatu zilizoleta upungufu wa chakula duniani zimewapa somo kama nchi kujipanga vizuri kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha ambapo wamechukua hatua mbalimbali kwenye kilimo kwa maana cha mazao,ufugaji na uvuvi pamoja na kulina asali.

Kwa kuongeza bajeti ya kilimo Kwa kuweka fedha nyingi katika sekta hiyo ili zikafanye wananchi wakalime zaidi,kuvuna zaidi,kukuza zaidi na kuwa na akiba kubwa ya chakula.

Hivyo ameeleza hatua nyingine kama serikali ilizochukua katika kukabiliana na changamoto hiyo ni pamoja na usajili wa wakulima ambao umeanza katika maeneo mbalimbali ili kujua nchi ina idadi ya wakulima wangapi ili waweze kuwahudumia.

Pia amesema jambo jingine ambalo wamelifanyia kazi ni ujenzi wa maghala ambayo wanaendelea kujenga lakini wanataka kila Mkoa ujenge maghala na yote watayakagua na kuyaweka kwenye kanzi data ya serikali na kujua kila ghala linauwezo wa kuchukua chakula kiasi gani ili kuhifadhi chakula kimkoa na endapo tatizo litatokea katika Mkoa kuwe na chakula cha kutosha kuwahudumia wananchi wake.

Vilevile hatua nyingine ni kuongeza thamani ya mazao kwa kuweka mazingira ya kuvutia sekta binafsi kuwekeza na kujenga viwanda vingi vya kukoboa na kuongeza thamani ya mazao wanayoyavuna ili waweze kukuza kwa bei kubwa.

“Ndani ya taifa letu kwa sasa tuna akiba ya chakula tani 250,000, kuanzia mwaka huu tunakwenda kumwaga fedha kununua chakula tunataka tuwe na hifadhi ya tani 500,000,ambazo tutahifadhi kwenye maghala yetu nimeisha mpa kibali Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha atoe fedha kwa ajili ya kununua chakula kwaio niwaombe wakulima msivushe mazao kwenda nje msubili Wizara inakuja kununua,”.

Sanjari na hayo ametumia fursa hiyo kuwaomba wakulima kuweka chakula cha kutosha kwa ajili yao na familia zao ili itakapotokea uhaba wa chakula Tanzania iwe imejiweka vizuri.

“Hesabu ya chakula kilichopo kwenye maghala ya serikali tani moja inahudumia watu 180 ambapo hesabu hii haikubaliki kabisa tunataka turudi tuwe na akiba ya chakula ambacho tani moja itahudumia watu 20 tu ndio maana tumeweka nguvu sana katika kununua chakula na akiba ya chakula tutachukua hatua kwa hatua mpaka tufike lengo ambalo tumeliweka la tani moja watumie watu 20 na siyo kama tulivyo sasa,”.

Mbali na hayo ameeleza kuwa duniani katika mfumuko wa bei kwa mazao ya mchele na mahindi ni asilimia 11 lakini nchini hapa kwa sababu ya mavuno bei zinakwenda zinateremka hivyo wanaenda kuweka jitihada mbalimbali ili kukuza kilimo.