February 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Samia, Balozi Nchimbi na Dkt. Mwinyi wapongezwa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

JUMUIYA ya kimataifa, hususan mabalozi wa nchi mbalimbali waliopo Tanzania, ikiwa ni pamoja na Uganda, Algeria, India na Marekani, wamepongeza uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Mbali na kumpongeza Dkt. Samia, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mabalozi hao pia wamewapongeza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuthibitishwa kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar.

Mabalozi hao walitoa pongezi hizo wakati wa mazungumzo yao na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, yaliyofanyika kwa nyakati tofauti leo Februali 12, 2025 katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Ahmed Djellal, aliangazia pia uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Algeria, hususan mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika. Aidha, alitoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia, Rais Dkt. Mwinyi na Balozi Nchimbi kwa kuaminiwa kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Balozi Nchimbi na Balozi Djellal pia wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Algeria kupitia sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa kiuongozi na fursa za masomo.

Katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey, ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na India umeendelea kuimarika na kunufaisha pande zote mbili, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, teknolojia na afya, Pia, alitoa pongezi kwa CCM kwa kuwaamini Rais Dkt. Samia, Rais Dkt. Mwinyi na Balozi Nchimbi kuwa wagombea wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Vilevile, katika mazungumzo kati ya Balozi Nchimbi na Naibu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, pande zote zimesisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Marekani katika nyanja mbalimbali, ambapo Lentz alitoa pongezi zake na kuwatakia kila la heri Rais Dkt. Samia, Rais Dkt. Mwinyi na Balozi Nchimbi kufuatia maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa CCM.

Kwa upande wake, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, amefikisha salamu za pongezi kutoka kwa Serikali ya Uganda na chama tawala cha NRM, akieleza kuwa Uganda inatambua na kuheshimu mchango wa Tanzania na CCM katika harakati za ukombozi wa Afrika. Alimhakikishia Balozi Nchimbi kuwa uhusiano wa kidugu kati ya Tanzania na Uganda utaendelea kuimarika kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Aidha Balozi Mwesigye amesisitiza kuwa urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na Uganda umejengwa juu ya misingi imara ya mshikamano wa kikanda, ushirikiano wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi, ambao utaendelea kuimarika kwa ustawi wa mataifa hayo mawili.