

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa Mahakama kuhakikisha kasi ya utoaji haki kwa wananchi inaendana na ubora wa jengo jipya la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania ambalo limejengwa kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Dkt.Samia ametoa kauli hiyo Leo April 5 mwaka huu jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo hilo sambamba na jengo la Utumishi wa Mahakama na Makazi ya Majaji ambayo yote kwa pamoja yamegharimu kiasi Cha shilingi bilioni 185.4.
Amesema kuwa na majengo mazuri ni kwa ajili ya kujenga mazingira mazuri ya utendaji kazi hasa ya utoaji haki kwa wananchi.
Dkt.Samia amesema,mazingira hayo mazuri yaendane na ubora wa huduma zinazotolewa katika majengo hayo .
Amesema ,Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa Majaji hapa nchini na kuwataka nao kufanya kazi ya utoaji haki bila kuangalia Hali ya mtu.
Aidha Dkt Samia ameipongeza Mahakama kwa ujenzi wa jengo hilo ambalo limezingatia matumizi ya TEHAMA huku akionyesha kufurahishwa na Mifumo ya Mahakama kusomana.
Amesema ,Mifumo hiyo inamwezesha mtu kuangalia mwenendo wa kesi katika mkoa wowote anaoutaka.
Ametumia nafasi hiyo kuhimiza Mahakama kuendelea kuifanya Mifumo yake kusomana Ili kurahisisha kazi ya utoaji haki na kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.
Amesema,kwa upande wa Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya Mahakama Kila mwaka Kutoka bilioni 161 Hadi shilingi bilioni 321 mwaka huu wa fedha kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Prof.Ibrahim Hamis Juma ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha Mahakama kupata jengo hilo zuri na hivyo Makao Makuu ya Mahakama kuhamia Dodoma.
“Tunashukuru mheshimiwa Rais kwa kuiwezesha Mahakama kufanya maboresho kupitia mipango yake ,bila uwezeshaji mipango yetu ingebaki kwenye makaratasi.”alisema Prof.Ibrahim
More Stories
Taasisi ya Tulia Trust yamfuta machozi bibi anayeishi kwa kuokota makopo
Askofu Masondole awataka vijana kutofuata mila na desturi zisizokubalika nchini
Dkt.Biteko :Mradi wa Kufua umeme wa JNHPP wakamilika rasmi