March 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia atimiza ndoto ya wananchi Same,Korogwe,Mwanga ya kupata maji

Martha Fatael,Timesmajira Online,Mwanga

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Samia Suluhu Hassan, ametimiza ndoto ya miaka 19 ya wananchi wa Wilaya za Same,Mwanga na Korogwe mkoani Kilimanjaro na Tanga ya kupata maji safi na salama.

Ndoto hiyo imetimia baada ya Rais Samia kuzindua rasmi mradi mkubwa wa maji Same,Mwanga na Korogwe utakaonufaisha zaidi ya wananchi 456,000 katika Wilaya hizo..

Sanjari na hayo Rais Samia amewataka wananchi wa mikoa hiyo na maeneo mengine nchini, kuhakikisha wanalinda miundombinu na vyanzo vya maji.

Mradi wa Same,Mwanga na Korogwe, unakamilisha historia ya miaka 19,hadi sasa umegharimu zaidi ya bilioni 406 za kitanzania.

Hata hivyo Dkt.Samia,amesema mradi huo pamoja na kusuasua hakuamini katika kushindwa na badala yake aliomba mkopo wa masharti nafuu kwa nchi za Saudi Arabia na Kuwait ambao ndiyo wafadhiliwa wa mradi huo,na sasa mradi umekamilika.

Kabla ya uzinduzi, Rais alikagua chanzo cha maji cha mradi huo bwawa la Nyumba ya Mungu na mtambo wa kuchuja maji kabla ya kusambaza kwa wananchi.

Kukamilika kwa mradi huo kunatimiza falsafa ya Rais Samia ya kumtua mwanamke ndoo kichwani aliyoitangaza mara kadhaa tangu kushika wadhifa wa Rais, Machi mwaka 2021.

Itakumbukwa Rais Samia aliweka jiwe la msingi la mradi huo, Novemba mwaka 2018,wakati akiwa Makamu wa Urais,huku upatikanaji wa maji kwa Wilaya hizo ukiwa chini ya asilimia 50.

Anasema mradi huo utakuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya hizo, kuboresha sekta ya elimu kwani wanafunzi hawatatumia muda mrefu kutafuta maji.

“Taarifa nilizonazo ni kwamba wananchi wanapata maji kwa saa 24 katika Wilaya hizi,sasa kama hili ni tofauti na uhalisia mniambie nishughulike na Waziri,” amesema Dkt.Samia.

Ameagiza vijiji vinne vinavyozunguka bwawa la Nyumba ya Mungu vuinganishwe katika mradi huo ili kuwapa ari ya kulinda mradi huo.

Hata hivyo Rais Samia amewataka wananchi wafungiwe mita(dira) za maji za kulipa kabla ya kutumia kadri uwezavyo kulingana na matumizi badala ya mfumo uliopo ambao watu wanatumia wawezavyo ndio wanalipa,hali inayochangia baadhi kuhisi wamebambikiwa bili.

Vilevile amesema,Serikali haihamsishi sekta binafsi kuingia katika sekta ya maji kwani wananchi hawataweza kulipia bali imewekeza katika eneo hilo ili kuwasaidia wananchi wake.

“Hii ni awamu ya kwanza, niombe wenzetu wa Korogwe wasiwe na hofu kwani awamu ya pili maji yatawafikia mapema iwezekanavyo,”.

Awali Katibu Mkuu waWizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri,amesema mradi huo ulibuniwa kutoa huduma katika vijiji 17 vya Wilaya ya Mwanga, vijiji 16 vya Same na vijiji 5 Wilaya ya Korogwe.

Akizungumzia mradi huo Waziri wa Maji Jumaa Aweso,amesema alipata wakati mgumu pale ambapo Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, aliposena mradi huo usipokamilika hadi kufika Juni mwaka jana angejiuzulu.

Amesema mradi huo umesanabisha baadhi ya watumishi wa Wizara ya Maji,kupoteza kazi ingawa sasa maji yanapatikana kwa Wilaya rhizo.

Aweso amesema vyama vya upinzani vilikuwa vikibeza utekelezaji wa mradi huo ambao sasa umefikisha asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mjini na vijiji.

Awali Mbunge wa Same Magharibi, Mathayo David,amesema wananchi wa Same wamefuraishwa na Serikali ambayo imetoa zaidi ya bilioni 340.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwamo mradi huo,pamoja na ujenzi vituo vya afya 3 na hospitali ya Wilaya ya Same.

Huku Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo, amesema mradi huo utaondoa changamoto kwa wananchi wa Wilaya hiyo na sasa watafanya shughuli za uchumi.

Ameomba fedha kwa ajili ya kuondoa magugu maji Ziwa Jipe ili kuendelea kupeleka maji katika bwawa la Nyumba ya Mungu.