Asema demokrasia ni kuheshimu matokeo na kuendelea kujenga Taifa; aonya wanaochochea vurugu
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuongoza Taifa kwa misingi ya amani, umoja na maendeleo endelevu baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Saba wa Tanzania katika sherehe zilizofanyika Chamwino, Dodoma, tarehe 3 Novemba 2025.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi, viongozi wa kitaifa na wageni wa kimataifa, Dkt. Samia alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kufikia hatua hiyo, na Watanzania kwa imani waliyoonesha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwa serikali inayoongozwa na chama hicho.
“Niwashukuru Watanzania wote kwa imani yenu kwa CCM, na kwa kutupa mimi na Makamu wa Rais fursa hii adhimu ya kuwatumikia. Uchaguzi umekwisha, sasa tuijenge nchi yetu na utu wa Mtanzania,” amesema Dkt. Samia.
Awapongeza washindani na waangalizi wa uchaguzi
Dkt. Samia almewapongeza wagombea wengine 17 wa nafasi ya urais kutoka vyama mbalimbali kwa kuendesha kampeni zenye hoja na kuepuka vurugu, akisema kuwa hilo linaonesha ukomavu wa kidemokrasia nchini.
Aidha, alitoa pongezi maalum kwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, na vyama vyote vya siasa kwa kukamilisha uchaguzi kwa amani. Amezipongeza pia taasisi za kimataifa kama Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC na ICGLR kwa kushiriki kama waangalizi wa uchaguzi na kutoa mrejesho wa ujenzi.

“Tumeusikia ushauri wa waangalizi na tutaendelea kufanya vizuri zaidi siku zijazo. Hata hivyo, kama alivyosema Hayati Benjamin Mkapa, maagizo tutayakataa, lakini ushauri mzuri tutauzingatia,” amesisitiza Rais Samia.
Aonya wachochezi wa vurugu
Katika hotuba yake, Rais Samia alionyesha masikitiko yake kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika baadhi ya maeneo nchini baada ya uchaguzi. Alibainisha kuwa baadhi ya wahusika wa vurugu hizo si raia wa Tanzania na akatoa onyo kali kwa wale wote wanaojaribu kuhatarisha utulivu wa nchi.
“Vurugu huishia kupimana nguvu, lakini mazungumzo huleta mshikamano. Kamati za Ulinzi na Usalama hakikisheni maisha ya wananchi yanarejea kawaida kuanzia leo,” amesema kwa msisitizo.
Atoa wito wa umoja na mshikamano
Rais Samia amewataka Watanzania wote kuacha tofauti za kisiasa na kuungana kujenga taifa, akisisitiza kuwa uchaguzi ni tukio la msimu mmoja ndani ya miaka mitano, lakini maisha na maendeleo ya nchi ni ya kudumu.

“Tuendelee kuilinda itikadi yetu ya umoja na mshikamano. Uchaguzi umeisha, sasa ni wakati wa kufanya kazi,”amesema.
Ameendelea kusisitiza falsafa ya 4R’s — Reconciliation, Resilience, Reforms, na Rebuilding — kama dira ya serikali yake katika awamu ya pili ya uongozi wake, akisema kuwa itakuwa msingi wa kuimarisha umoja wa kitaifa na maendeleo.
Ataka hekima, upendo na uvumilivu
Rais Dkt. Samia alitumia jukwaa hilo kuhimiza Watanzania kuchagua busara na upendo badala ya chuki na vurugu, akisema demokrasia haipimwi kwa nani kashinda uchaguzi, bali kwa jinsi taifa linavyoshirikiana baada ya uchaguzi.
“Niwasihi Watanzania tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemuko, upendo badala ya chuki, na amani badala ya vurugu. Taifa letu ni kubwa kuliko mtu yeyote,” amesema kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa Serikali, vyama vya siasa, jumuiya za kiraia, na taasisi za dini zote zina jukumu la kuendeleza mazungumzo na maridhiano kwa manufaa ya nchi.
Atoa shukrani na ahidi kazi zaidi
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuhimiza amani kipindi chote cha uchaguzi na kuahidi kutoa dira ya miaka mitano ijayo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Safari ya kuwatumikia Watanzania kwa kipindi cha pili inaanza rasmi leo. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania,”amesema akihitimisha hotuba yake huku ukumbi wa Chamwino ukishangilia kwa makofi.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi