Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Morogoro
VIJANA wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), UVCCM Wilaya ya Kilombero Jimbo la Mlimba Mkoa wa Morogoro, wamepatiwa baiskeli 16 kwa jili ya kazi za kuimarisha chama mkoani humo.
Baiskeli hizo zimetolewa na mjumbe wa kuhakiki mali na ujenzi wa ofisi za chama hicho Wilaya nzima ya Kilombero, Dkt. Rose Rwakatare ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shule za St Mary’s nchini.
Hafla ya kukabidhi baiskeli hizo ambazo zitagawanywa katika Jimbo la Mlimba ilifanyika jana katika ofisi za CCM Wilaya ya Kilombero na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kupokea baiskeli hizo, Katibu wa CCM Wilaya ya Kilombero, Emmanuel Ebenezer, amemshukuru Dkt. Rose kwa msaada huo ambao alisema utasaidia kazi za kuimarisha chama hicho.
Amesema baiskeli hizo zitagawanywa katika kata 16 za Jimbo la Mlimba ambapo makatibu wa UVCCM kata watakuwa wakizitumia kwenye kazi zao za chama.
“Hizi baiskeli ni za chama si mali ya mtu binafsi kwa hiyo unaitumia nafasi yako ikikoma unaiacha anayekuja anaitumia na mhakikishe zinatunzwa kwaajili ya shughuli za chama tunamshukuru sana mdau wetu wa chama Dk. Rose Rwakatare,” alisema
Amesema vijana wa UVCCM Mlimba wamekuwa na changamoto kubwa ya usafiri kwa muda mrefu hivyo baiskeli hizo zitatoa mchango mkubwa kwenye kuimarisha shughuli za chama mkoani humo.
Kwa upande wake, Dkt. Rwakatare alisema anafuraha kutimiza ahadi yake ambayo aliitoa kwa muda mrefu na kwamba anaamini vijana sasa wamepata nyenzo ya kuwasiadia kuimarisha chama hicho.
“Vijana walikuwa wanalalamikia usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine sasa kupatikana kwa usafiri huu ni ukombozi kwao na mimi najisikia fahari sana kutimiza ahadi yangu leo hii,” amesema Dk. Rose.
Mmoja wa vijana hao, Jackson Edward alimshukuru Dk. Rwakatare kwa msaada huo ambao alisema vijana wengi wa UVCCM walikuwa wakiisubiri kwa muda mrefu.
Amesema Wilaya ya Mlimba ina kata 16 hivyo kwa kila kata kupatiwa baiskeli moja kutawasaidia makatibu wa UVCCM kuzunguka sehemu mbalimbali kwaajili ya kujenga chama hicho.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote