December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Pindi Chana aweka jiwe lamsingi jengo la jiolojia Karatu

Na Sophia Fundi, Timesmajira Online, Karatu

WAZIRI wa maliasili na utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ameweka jiwe la msingi mradi wa makumbusho ya kisasa ya jiolojia yanayojengwa katika eneo la Njiapanda wilayani Karatu.

Mradi huo ambao unafadhiliwa na serikali ya jamhuri ya China, wenye hadhi ya kimataifa umewekewa jiwe la msingi Novemba 16 mwaka huu, katika hafla fupi iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo balozi wa China nchini Tanzania.

Akizugumza mara baada ya tukio hilo, Balozi Dkt. Pindi Chana aliishukuru serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa ushirikano wa nchi hizo mbili kwa ufadhili wa mradi huo.

Dkt. Chana amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika Mei, 2025 na utagharimu kiasi cha Tsh. bilion 25 fedha zinazofadhiliwa na serikali ya Jamhuri ya China.

Waziri wa maliasili na utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana (wa pili kutoka kushoto), akiweka jiwe la msingi jengo la makumbusho ya jiolojia linalojengwa wilayani Karatu mkoani Arusha.

Kwa upande wake Kamishna wa hifadhi ya Ngorongoro Elirehema Doriye amesema mradi huo wa Makumbusho ya Jiolojia utakapokamilika utasaidia watalii kutoka mataifa mbalimbali kufurahia zao la utalii wa miamba kutokana na vivutio vitakavyokuwa katika makumbusho hiyo.

Doriye amesema, mradi huo utaongeza kipato cha utalii kwani utakuwa na vivutio vya kisasa na pia utasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya za Karatu, Ngorongoro, Longido pamoja na Monduli.

Akitoa taarifa ya mradi mbele ya Waziri, afisa uhifadhi mkuu anayesimamia idara ya urithi wa utamaduni na Jiolojia, PCO Dkt. Agness Gidna ameeleza kuwa makubusho hiyo itakapokamilika itakuwa na maelezo ya vivutio mbalimbali.

Vivutia hivyo kiwemo urithi wa Jiolojia unaopatikana katika eneo la Ngorongoro,taarifa zilizohusu milima na mabonde,kreta za Ngorongoro zilivyotokea, wanyama waliopo, mioto ya asili, mito na maji na umuhimu wake kwa jamii zinazozunguka Ngorongoro.

Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema utekelezaji wa mradi huo unatokana na mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili Tanzania na China, ndio unaoleta matokeo ya kuboresha miundombinu ikiwemo Sekta ya utalii.

Akizungumza katibu mtendaji wa UNESCO Tanzania Prof. Hamis Malebo ameeleza hifadhi ya miamba ya Ngorongoro ndio hifadhi kubwa na yenye maajabu makubwa barani Afrika, kutokana na uwepo wa kreta mbili za ajabu na volcano hai ambapo nchi ya Tanzania ni ya pili barani Afrika, kuwa na hadhi ya Jiopak inayotambuliwa na UNESCO ikitanguliwa na Morocco.