March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Pima awataka wakuu wa shule kusimamia nidhamu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora

WALIMU Wakuu wa shule za msingi na sekondari zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wameagizwa kusimamia nidhamu za walimu na wanafunzi katika shule zao ili kuinua taaluma.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt.John Pima wakati akifunga semina maalumu ya Maofisa Elimu, Walimu wa Nidhamu, Waratibu na Wakuu wa shule zote mjini hapa.

Amesema serikali imefanya maboresho ya miundombinu katika shule zote za Manispaa hiyo hivyo kufanya mazingira ya ufundishaji na kujifunza kuwa bora.

“Mazingira bora yaliyopo katika shule zetu ni chachu ya kuwezesha watoto wetu kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya kitaifa hivyo kuongeza ufaulu katika manispaa yetu, katika hili ni lazima tuimarishe nidhamu,” amesema Dkt.Pima

Dkt.Pima ameahidi kutoa motisha kwa kila mwalimu ambaye somo lake litapata alama A za ufaulu kwa idadi yoyote ile ya A, aidha, Walimu wakuu na shule itakayoongoza kwa ufaulu nao watapata zawadi.

Pia amewataka kusimamia fedha zote zinazopelekwa katika shule zao ili zifanye kazi iliyokusudiwa na thamani ya fedha ionekane, kinyume na hapo hatua za kiutumishi zitachukuliwa kwa yeyote atakayekwamisha.

“Tunatumia fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya elimu katika shule zetu, miradi hii ni lazima itekelezwe kwa wakati na iwe na ubora unaotakiwa,hatutamfumbia macho Mkuu wa shule yeyote atakayezembea,”amesema Dkt Pima.

Akisoma maazimio ya semina hiyo, Mratibu Elimu Kata ya Mwinyi,Mwalimu Raphael Mageni,amesema kuwa shule kwa kushirikiana na wazazi,walezi na wadau watahakikisha wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana shuleni.

Pia wamekubaliana kutokomeza utoro wa wanafunzi katika shule zao na kuwa na mfumo wa mitihani ya pamoja kwa shule zote zilizopo katika halmashauri hiyo ili kuongeza weledi na ushindani katika ufundaji watoto.

Aidha amesema kuwa watasimamia miradi inayotekelezwa katika shule zao pamoja na nidhamu na uadilifu wa walimu na wanafunzi na kuwapa watoto elimu ya kujitegemea.