December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nkullo:Madarasa ya UVIKO 19 yameongeza uandikishaji darasa la elimu ya awali ,darasa la kwanza Kongwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Kongwa

HALMASHAURI  ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma imefanikiwa kuvuka lengo la uandikishaji wanafunzi wa elimu ya darasa la awali pamoja na darasa la kwanza mwaka huu.

Kuwepo kwa mazingira rafiki ya kisera nchini Tanzania kumepelekea ongezeko la uandikishaji wa watoto katika elimu ya awali kufikia 500,000 ndani ya mwaka mmoja kutoka 1,069,823 mwaka 2015 mpaka 1,562,770 mwaka 2016 na kufanya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza nchini kuongezeka kwa asilimia 411 kutoka watoto 1,404,998 mwaka 2012 mpaka watoto 2,120,667mwaka 2016 huku zaidi ya nusu ambayo ni asilimai 54.8 ya watoto walioandikishwa darasa la kwanza wana elimu ya awali.

Aidha katika mwongozo wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM),serikali imepanga kuhakikisha inatekeleza programu hiyo ili kushughulikia kikamilifu mahitaji yote yakiwemo ya elimu kwa maendeleo ya watoto wenye umri wa kuanzia miaka sifuri hadi minane.

Akizungumza na mtandao huu ofisini kwake ,Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt.Omary Nkullo amesema, ujenzi wa madarasa ya UVIKO 19 ambayo yamejengwa katika shule shikizi wilayani humo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi hiyo ya uandikishaji .

Dkt.Nkullo amesema hadi Machi 31 mwaka huu walikadiria kuandikisha watoto wa darasa la awali 16,767 lakini hadi Februari 25 mwaka huu walikuwa wameshaandikisha watoto 11,455 ambayo ni sawa na asilimia 68 .

“Hadi itakapofika Machi 31 naamini tutakuwa tumevuka lengo la uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya darasa la awali.”amesema Dkt.Nkullo

Kuhusu uandikishaji wa darasa la kwanza Mkurugenzi huyo amesema,walikadiria kuandikisha wanafunzi 16,074,lakini  hadi Februari 25 mwaka huu walikuwa wameshaandikisha wanafunzi 14,002 sawa na asilimia  87.35 ya lengo .

“Hii imewezekana kutokana na kuwepo kwa miundombinu ya kutosha ambayo imeleta mwitikio  kwa wazazi kuwapeleka watoto kuandikishwa shule .”amesisitiza Dkt.Nkullo na kuongeza kuwa

“Kipindi cha nyuma kabla ya kujengwa kwa madarasa ya UVIKO 19,hali ya uandikishaji wa wanafunzi kwa makundi hayo ilikuwa ni kati ya wanafunzi 9000 hadi 11,000.”

Hata Dkt.Nkullo amesema licha ya mafanikio hayo lakini bado kuna changamoto ya baadhi ya watoto kutoandikishwa darasa la awali na darasa la kwanza kutokana na baadhi ya watoto wanaopaswa kwenda darasa la kwanza ,kupelekewa kufanya kazi za ndani lakini pia baadhi ya wazazi kuhama na watoto waliofikia kuandikishwa shule kwa ajili ya shughuli za kilimo na kufuata malisho ya mifugo.

“Kama unavyojua,kuna fedha za Rais Samia Suluhu Hassan za UVIKO 19 ambazo tulipewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule za msingi na sekondari,madarasa haya yameongeza uandikishaji  wa watoto wa elimu ya awali,

“Lakini pamoja na watoto wengi kuandikishwa hadi kuvuka lengo la uandikishaji tulilokuwa tumejiwekea lakini bado tunayo changamoto kwa baadhi ya watoto ambao wazazi wao huhamia mashambani na kurejea ni mpaka mwezi Mei au Juni.”amesema Dkt.Nkullo

Moja ya madarasa yaliyojengwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma kwa fedha za UVIKO 19

Mtaalam wa masuala ya elimu ya awali Lyambwene Mutahabwa  amesema mtoto ni rasilimali muhimu chini ya jua ambaye anapaswa kuwekewa mazingira tangu akiwa mdogo ili kumjenga katika Malezi,makuzi na maendeleo yake.

“Kwenye elimu ya awali tunasema miaka minane ya kwanza katika maisha ya mwanadamu  hujenga msingi bora kwa ajili ya masomo ya ngazi zinazofuata kwa ajili ya maisha yake yote yaliyosalia hapa duniani…,kwa hiyo ukiboronga katika kipindi cha umri huo wa mtoto unakuwa umemjengea mtoto kushindwa na kuwa na  anguko kubwa huko aendako ,

“Kama jamii lazima ijue kwamba msingi wa mtu mzima unawekwa wakati wa miaka minane ya kwanza ya maisha ya binadamu .”

Kwa mujibu wa Afisa Elimu wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa Eugen Shirima amesema,madarasa yaliyojengwa kwa fedha za UVIKO 19 yameleta chachu wilayani humo na kupelekea wazazi wengine kuamua kuanzisha ujenzi wa shule shikizi 10.

“Baada ya wananchi wa vitongoji vingine kuona wenzao waliokuwa wana shule shikizi wamepata fedha za serikali na kujenga madarasa,nao wameamka na kuanza ujenzi wa shule shikizi ambao utasaidia kwa watoto wengi zaidi kuandikishwa darasa la awali na darasa la kwanza.”amesema aeaugin na kuongeza kuwa

“Wananchi hao wanaamini wenzao wamepata fedha na kujengewa madarasa lkutokana na mwanzo waliokuwa wameuanzisha wa kujenga madarasa angalau ya kuanzia.”

Shirima amesema kufuatia ujenzi wa madarasa hayo ya fedha za UVIKO 19,sasa wanakamilisha ujenzi wa matundu ya choo ili shule shikizi zilizopata madarasa hayo ziweze  kuwa na vigezo vya kusajiliwa na kuwa shule kamili na watoto waanze kusoma kuanzia darasa la awali mpaka darasa la saba.

Naye Mratibu Elimu Kata ,Kata ya Sejeli  ambayo imepata majengo mapya katika kitongoji cha Muungano Francis Lukosi amesema ,ujenzi wa madarasa hayo umeongeza ari ya wazazi katika uandikishaji wa watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza kutokana na huduma ya shule kusogezwa karibu na wananchi.

Miongoni mwa madarasa yaliyijengwa kwa fedha za UVIKO 19 katika kitongoji cha Muungano katika kijiji cha Sejeli wilayani Kongwa mkoani Dodoma

Amesema,awali kabla ya kujengwa kwa madarasa kulikuwa na vyumba vichache  vya madarasa ambayo hayakuwa na ubora ambayo yalijengwa kwa nguvu za wananchi ili angalau watoto wa darasa la awali waweze kusoma karibu kwani haikuwa rahisi watoto hao kutembea umbali mrefu kufuata shule mama katika kijiji cha Sejeli.

Vile vile amesema,kusogezwa  huduma ya shule karibu na wananchi kumeongeza  ari ya wanafunzi kuhudhuria masomo  tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya ujenzi wa madarasa hayo ambapo uandikishaji ulikuwa mdogo lakini hata wale walioandikishwa wengi walikuwa wakiacha shule hasa walipokuwa wakiingia darasa la tatu kwani huwapasa kutembea umbali wa kilomita 8 hadi 9 kufuata shule mama katika kijiji cha Sejeli wilayani Kongwa.

“Kutoka kijiji cha Sejeli mpaka kitongoji cha Muungano ambacho ndiko kuna shule shikizi ni kilomita 8 hadi 9 ,sasa utaona kwamba huu ni umbali mrefu sana kwa watoto hasa wale wadogo wa darasa la tatu ,kwa hiyo madarasa haya yamesaidia sana kwani kwani baada ya kumalisha hatua za usajili watoto wote kuanzia darasa la awali hadi sarasa la saba watasoma katika kitongoji chao ambapo shule ipo.”amesema Lukosi

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Sejeli ambayo ndiyo shule mama ya shule shikizi ya Muungano Susan Jonas amesema tayari wameshaanza utaratibu wa kutengeneza zana ili kulifanya darasa la awali kuwa darasa linaloongea kwa lengo la kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi.

Mwananchi wa kijiji cha Sejeli Elizabeth Charles ameishukuru Serikali kwa kujenga majengo ambayo sasa yanaenda kutatua changamoto ya umbali ambayo ilikuwa ni adha kubwa kwa wanafunzi wadogo hususan wa darasa la tatu na wanafunzi wote kwa ujumla kutembea umbali mrefu .

Mwalimu wa darasa la awali katika shule shikizi  ya Muungano katika kitongoji cha Muungano Stellah Moma amesema pamoja na uandikishaji wengi wa watoto darasa la awali lakini pia madarasa hayo yameongeza muamko wa wazazi hata kushiriki katika kazi za kutengeneza zana za ujifunzaji  wa watoto shuleni hapo kwa kushirikiana na mwalimu huyo.