May 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Ndumbaro:Rais Samia ameweka historia kufanya Urekebu wa sheria kwa kutumia fedha na wataalamu wa ndani

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WIZARA ya Katiba na Sheria imesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya Urekebu wa Sheria kwa kutumia fedha za ndani na wataalamu wa ndani.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Mei 20,2025 na Waziri wa Wizara hiyo,Dkt.Damas Ndumbaro wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema kwa wanasheria wanaoijua sheria na wanaojua historia ya sheria wanajua kuwa hilo jambo kubwa zaidi kuwahi kufanywa na Rais aliyekuwepo madarakani kwakutumia fedha za ndani na wataalamu wa ndani na kufanywa kwa ustadi mkubwa.

Dkt.Ndumbaro amesema kuwa sheria hiyo iliyofanyiwa urekebu na kukamilishwa zoezi lake Aprili 23,2025 Chamwino-Dodoma zitaanza kutumika rasmi Julai Mosi Mwaka huu.

Aidha amesema kuwa kwahivi sasa sheria  zote zinasomeka kwenye kurasa moja.

“Ndipo muone sasa sekta ya sheria imeiva,imeiva kwa wataalamu,imeiva kwenye Rasilimali nyingine na zoezi hilo lilipata baraka za mwisho kabisa kwasababu kwa mujibu wa sheria ile imewataja watu wa nne,”amesema Dkt.Ndumbaro.

Pamoja na hayo Dkt.Ndumbaro amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA katika utoaji huduma za kisheria ambapo hadi kufikia Aprili,2025 asilimia 75 ya mifumo ya TEHAMA katika Sekta ya Sheria imeunganishwa.

Pia amesema Wizara imeimarisha matumizi ya mfumo wa Portal ya HAKI SHERIA ambao unatumiwa na wananchi na maafisa Dawati la Msaada wa Kisheria katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 nchini. 

Vilevile amesema ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na gharama nafuu, Serikali imeendelea kufungua ofisi mpya za Mashtaka katika Wilaya ambapo ofisi hizo zimeongezeka kutoka 53 mwaka 2021 hadi 108 mwaka 2025.

Hata hivyo Waziri huyo amesema kuwa Wizara inatekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambapo tangu kuzinduliwa kwa Kampeni hiyo Aprili, 2023, jumla ya Mikoa 25 imefikiwa na kampeni.

“Ili kuhitimisha nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara, Mkoa wa Dar es Salaam kampeni itatekelezwa Juni, 2025.

“Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia umefanyika katika mikoa mitatu na hivyo kukamilisha maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isipokuwa Dar es Salaam.

Amesema kuwa kupitia Kampeni hiyo, jumla ya Halmashauri 180, Kata 1,907 na Vijiji/Mitaa 5,702 ilifikiwa na jumla ya wananchi  2,698,908  walifikiwa na kupata elimu na huduma za kisheria kupitia mikutano ya ana kwa ana.