November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Ndumbaro: Watanzania onesheni uzalendo Ligi ya Mabingwa Afrika

*Goli la mama sasa Mil. 10/-

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

WATANZANIA wametakiwa kuweka uzalendo na utaifa mbele kwa kuziunga mkono na kutoa hamasa kwa timu za Yanga na Simba katika michuano yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Rai hiyo ilitolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa kikao cha Serikali na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), sanjari na viongozi wa klabu za Simba na Yanga kuweka mikakati ya ushindi.

Klabu ya Simba inatarajiwa kushuka dimbani dhidi ya Al ahaly ya Misri katika mchezo utakaopigwa Machi 29 mwaka huu, wakati klabu ya Yanga itashuka dimbani dhidi ya Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini katika mchezo utakaofanyika Machi 30, 2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ndumbaro alisema, Watanzania wanatakiwa kufanya mambo mawili ambayo ni kutoa hamasa kujaza uwanja na kuweka uzalendo katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya Ligi hiyo.

“Tumefanya kikao kati ya Serikali, TFF, Bodi ya Ligi na viongozi wa timu ya Yanga na Simba, tumewasisitiza kuweka uzalendo na utaifa kwanza.

“Simba na Yanga zinaiwakilisha nchi, tunaomba kushirikiana na Serikali ili kupata mafanikio, zitasema ifanye nini ili zifanye vizuri, sisi Kwa upande wetu tumeweka mambo sawa ikiwamo Uwanja na usalama,”amesema Dkt. Ndumbaro.

Aliongeza kuwa” Rais wetu yupo tayari kusaidia michezo kimataifa na ameongeza dau la goli kutoka milioni tano na sasa milioni 10.

“Lengo la kufanya hivyo ili timu zetu zifanye vizuri, kwani Serikali inatamani zifike fainali, ili ndoto hizi zitimie watanzania wanatakiwa kuunga mkono,”alisema.

Amewataka viongozi wa vilabu hivyo kwenda kuzungumza na wasemaji wa timu hizo kutokubeza michezo hiyo.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia alisema, timu za Yanga na Simba wakiingia nusu fainali wataongeza alama kwa Tanzania na klabu zao zitakazowezesha kwa idadi ya ushiriki wa timu nne katika msimu unaokuja katika michuano hiyo.