March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Nchimbi ‘atema cheche’ kwenye ufungaji wa kampeni

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

MGOMBEA Mwenza wa kiti cha Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewasihi wananchi wote kujitokeza kwa wingi kesho Oktoba 29, 2025 kupiga kura na kumchagua mgombea Urais wa chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wake.

Dkt. Nchimbi amesema hayo leo Oktoba 28, 2025 kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni za mgombea Urais wa chama hicho uwanja wa CCM Kirumba, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Dkt. Nchimbi, amemuhakikishia mgombea Urais Dkt. Samia, kuwa katika mikoa yote 25, ambayo alipita na kufanya mikutano ya kampeni wananchi wameonesha imani waliyonayo kwake.

Pia ameeleza kuwa, imani hiyo ya wananchi imetokana na utendaji kazi mzuri uliofanywa na Dkt.Samia, pamoja na utekelezwaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

“Katika kipindi cha uongozi wako umeendelea kuniteua na kuwa msaidizi wako, ambapo ulinichagua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, baadae ulinichagua kuwa Katibu Mkuu wa CCM na mwaka huu ukanichagua kuwa mgombea mwenza, hiyo yote inaonesha imani yako uliyonayo kwangu,”amesema Dkt.Nchimbi.

Aidha, Dkt. Nchimbi ameahidi kuendelea kumsaidia Rais Dkt. Samia kwa kuwatumikia wananchi na kusimamia ilani ya CCM 2025-2030, pamoja na kuendelea kusisitiza amani na utulivu nchini.

Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimehitimishwa leo na mgombea wa Urais kupitia chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezungumza na wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla uwanja wa CCM Kirumba, tayari kwa ajili ya kupiga kura kesho Oktoba 29, 2025.