March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nchimbi afanya mazungumzo na Katibu wa UDA nchini Kenya

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Kenya na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama Cha United Democratic Alliance (UDA), Hassan Omary.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika Juni 18,2025 katika Ofisi za makao makuu ya UDA, jijini Nairobi, ni mwendeleozo wa hatua mbalimbali ambazo CCM inachukua katika kudumisha ushirikiano wa kimkakati na vyama rafiki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EAC),Afrika na dunia kwa ujumla.

Aidha mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano wa kindugu kati ya vyama hivyo, kubadilishana uzoefu na mbinu bora za ujenzi wa chama cha siasa, uhamasishaji wa wanachama pamoja na kuendelea ushiriki wa wananchi katika demokrasia ya vyama vingi na utangamano wa Afrika Mashariki.

Katika taarifa iliyotolewa Juni 19, 2025 na Kaimu Katibu wa Habari wa Katibu Mkuu wa CCM, Aboubakary Liongo, imeelezwa kuwa, CCM inatambua kuwa uhusiano wa vyama vya siasa ni daraja la kuimarisha mshikamano na kuhimiza maendeleo ya pamoja ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Huku kikiendelea kulinda maslahi ya taifa na kukuza diplomasia ya vyama rafiki na manufaa ya wote.

Pia CCM kinatoa shukrani kwa UDA kwa mapokezi mazuri kwa Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Nchimbi na kubadilishana uzoefu kati vyama hivyo viwili ambavyo ni vyama tawala.