September 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwinyi mgeni rasmi kongamano wiki ya tathmini na ufuatiliaji

I

Na Mwandishi Wetu-Dodoma

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametoa wito kwa wadau wa ufuatiliaji na tathmini nchini kushiriki Kongamano la Tatu la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathimini na Kujifunza linalotarajiwa kufanyika kuanzia Sept 17 hadi 20 , 2024 Zanzibar.
Dkt. Yonazi amesema hayo wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake kuhusu masuala ya ufuatiliaji na tathimini katika maendeleo ya nchi.
Akizungumza kuhusu kongamano hilo, Dkt. Jim ameeleza kuwa, kongamano hilo linatoa fursa kwa wadau wote, ikiwemo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, na washirika wa maendeleo, kushirikiana kikamilifu katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini.
Aidha, amebainisha kuwa, kongamano la kitaifa ya wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) nchini Tanzania limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha eneo la Ufuatiliaji na Tathmini serikalini kwa kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathimini.
“Kupitia warsha, mafunzo, na midahalo, washiriki hujifunza mbinu mpya, zana, na teknolojia za kisasa za ufuatiliaji na tathimini ambazo zinaweza kutumika kuboresha utendaji wa miradi ya maendeleo” ameeleza Dkt. Jim.
Vilevile ameongeza kuwa, kongamano hilo linalenga kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo, kwa kuleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa serikali, wabunge, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi, aidha, linatoa jukwaa la kujadili jinsi ufuatiliaji na tathimini inaweza kutumika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na uwajibika.
Mbali na hayo Dkt. Yonazi ameeleza umuhimu wa ufuatiliaji na tathmini katika maendeleo ya nchi ya kwamba inachangia kwa namna mbalimbali katika kuboresha utendaji wa serikali na sekta binafsi.
“Ufuatiliaji na tathmini husaidia kubaini jinsi rasilimali zinavyotumika, na kuhakikisha kwamba fedha na muda zinalenga malengo yaliyokusudiwa, hii inasaidia kuongeza uwazi katika utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo, vilevile kwa kutumia data sahihi, watunga sera wanaweza kuchambua jinsi programu za maendeleo zinavyotekelezwa na matokeo yanayopatikana, hii husaidia kufanya maamuzi ya sera yaliyo sahihi zaidi kwa kuzingatia ushahidi wa kiutendaji” amebainisha
Aidha, ameongeza kuwa, ufuatiliaji na tathimini unawezesha serikali na wadau wa maendeleo kupima mafanikio na changamoto za miradi mbalimbali ya maendeleo, matokeo hayo pia yanatumika kurekebisha au kuboresha miradi na programu zinazoendelea kutekelezwa.
Sambamba na hayo alituma fursa hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali kushiriki katika kongamano kwa kuzingatia tija kubwa ya uwepo wa kongamano hilo na namna lilivyoratibiwa kwa ubora huku akizitaja faida ikiwemo; kuongeza uelewa juu ya masuala yua Ufuatiliaji na Tathmini, kupata maarifa juu ya ubunifu mbalimbali pamoja na kushirikishana uzoefu katika masuala ya ufuatiliaji na tathmini nchini.
“Ni wakati sahihi kwa kila mdau kushiriki kongamano hili la tatu, kwani tunaamini kukutana kwa wataalm wa masuala ufuatiliaji na tathmin kutaleta chachu katika utendaji wetu, na kutoa fursa ya kujitathmini ili kuendelea kuboresha maneno yenye udhaifu pamoja na kushirikishana uzoefu kupitia mada zitakazowasilishwa katika Kongamano letu muhimu,” alisisitiza Dkt. Yonazi
Awali
Mgeni Rasmi katika Kongamano la Tatu la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi.Kongamano linalotarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip uliopo Uwanja wa Ndege Zanzibar kuanzia tarehe 17 hadi 20 Septemba, 2024.Kongamano hilo limebebwa na kaulimbiu isemayo; “Kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia katika ufuatiliaji na tathmini,”.