Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi ameelezea kufurahishwa na kasi ya utatuzi wa kero za Muungano inayoonyeshwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo na mwenzake wa Zanzibar, Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dk. Halid Salumu Mohamed.
Aliyasema hayo jana kwenye mkutano baina yake na viongozi wakati wa ziara maalumu ya kikazi iliyofanywa na Waziri Jafo Ikulu Mjini Zanzibari.
Mazungumzo yao yalijikita kwenye mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi kifupi kwa shughulikia hoja 11 za Muungano pamoja na kazi kubwa inayo endelea ya kumalizia hoja saba za Muungano zilizobaki.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Dk. Hussein Mwinyi alimpongeza Waziri Jafo na Dk. Halid Salumu Mohamedi kwa ushirikiano wao mkubwa na kuchapakazi kwa kasi hadi kuwezesha kuondoa hoja 11 za Muunangano kati ya 18 zilizokuwa bado hazijapata ufumbuzi hapo awali.
Dk. Mwinyi alipongeza pia juhudi kubwa zinazofanywa kwa upande wa mazingira na amekubali suala la Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo cha mkoani Dodoma kwenda kufungua tawi Mjini Zanzibar, kwani kitasaidia kujenga viongozi na wataalam katika masuala ya Serikali za mitaa.
Licha ya pongezi hizo, Dk. Mwinyi alielekeza na kusisitiza kuendeleza kasi katika kushughulikia hoja zilizobaki za Muungano na ushirikiano katika kushughulikia masuala ya mazingira.
Katika kikao hicho Waziri Jafo alimshukuru Rais Mwinyi kwa kikao hicho kizuri na msaada mkubwa anao wapatia katika kutimiza majukumu aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kushughulikia masuala ya Muungano.
Pia alimshukuru Waziri kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa ushirikiano mkubwa anaompa katika kushughulikia hoja mbalimbali za Muungano.
Aidha, Jafo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa imani yao juu yake na kwa kazi kubwa wanayo ifanya ya kuimarisha Muungano na kuwaletea maendelea wananchi wa Tanzania wakiweko wananchi wa Ugunja na Pemba.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza wa Uwakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Merry Maganga, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mohamed Hamis Abdullah, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais na maafisa mbalimbali wanao shughulikia masuala ya Muungano.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu