December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Mwinyi akisalimia wananchi.

Dkt. Mwiny ateta na viongozi wa dini, awaahidi kutokomeza ubagizi Z’bar

Na Is-Haka Omar,TimesMajira, Online, Zanzibar

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dkt. Hussein Ali Mwinyi,ameahidi kupambana na vitendo vyote vya ubaguzi ndani ya jamii pindi akipata ridhaa ya kuongoza Zanzibar.

Amesema ili kutokomeza vitendo vya ubaguzi visiwani humo, lazima alikiri na kukubali kuwa vitendo hivyo vipo, kisha achukua hatua ya pili ya kutokomeza vitendo hivyo.

Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Zanzibar katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni, leo.

Amesema nchini kuna ubaguzi wa dini,ubaguzi wa kijinsia,ubaguzi wa kikanda wa Ubara, Uunguja na Upemba na yote hayo yanatakiwa kutokomezwa.

Amesema changamoto hizo zikiondolewa Zanzibar itaimarika kwa kasi kiuchumi, kijamii na kisiasa. Alisema viongozi na waumini wa dini ni wadau wakubwa wa maendeleo, hivyo wanatakiwa kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Dkt. Mwinyi amesema lengo lake kugombea urais ni kutaka kuwaletea wananchi wa makundi yote maendeleo endelevu. Alisema dhamira yake ni njema ya kuwatumikia wananchi wote, kwani kiongozi yeyote anayetafuta uongozi mkubwa wa nchi hawajibiki kwa wale wanaompigia kura tu, bali anawajibika hata kwa Mungu.

Amesema katika uongozi wake atahakikisha anatenda haki kwa makundi yote. Pia aliahidi kusimamia haki ya kikatiba ya kuhakikisha kila mtu anapata uhuru wa kuabudu dini anayoiamini ili nchi ibaki kuwa salama.

“Nia yangu ni kutenda haki kwa wote na naamini Mwenyezi Mungu atanijalia nitekeleze nia yangu kwa vitendo,” amesema Dkt.Mwinyi.

Alitumia nafasi hiyo kujiombea kura na kuwaombea wagombea wote wa CCM ili chama kishinde na kuendelea kuongoza dola. Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt.Abdulla Juma Mabodi,aliwambia waumini hao kuwa Dkt.Hussein amekuwa kiongozi mwenye sifa kubwa ya uongozi uliotuka na mcha Mungu.

Amesema mgombea huyo ana nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi hivyo waumini hao na jamii zao wahakikishe wanaompigia kura nyingi za ndio yeye pamoja na viongozi wote wa CCM.

Naye Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter aliwaambia waumini hao kuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dkt Mwinyi ni mgombea mwenye sifa ya unyenyekevu, mbunifu na mchapakazi na yupo karibu na watu.