December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango:Huduma za Posta zifike kwa jamii bila kujali walipo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango, amelitaka Shirika la Posta Tanzania  kuhakikisha huduma zake zinafika kwa jamii kwani ndio malengo ya kuanzishwa kwa shirika hilo.

Dkt.Mpango ameyasema hayo leo jijini hapa ,wakati akizungumza katika  maadhimisho ya siku ya Posta Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 9,kila mwaka ambayo mwaka huu kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma.

Amesema,shirika hilo linafanya kazi ya kuwahumia wananchi kwa niaba ya Serikali hivyo ni lazima lihakikishe linaigusa jamii ya watanzania kihuduma bila kujali mahali walipo.

Hata hivyo Dkt.Mpango amelipongeza shirika hilo kwa kufanya mageuzi makubwa ndani ya shirika hilo kwa kuleta huduma  mbalimbali zinazoakisi matumizi ya teknolojia katika kuwahudumia Watanzania.

“Nawapongeza sana kwa mageuzi hayo,lakini pia nafurahi kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya malengo makuu ya Umoja wa Posta Duniani na malengo yetu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na yale ya Sera ya Taifa ya Posta ya 2003 hasa katika kuwahudumia wananchi,”amesema Dkt.Mpango na kuongeza kuwa

“Tumeshuhudia shirika likibadilisha namna ya utoaji huduma zake kwa jamii kulingana na mahitaji na ndio maana wanashuhudia  Posta kuwa ya kidigitali na kuweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa urahisi ,tunahitaji kuwa na utendaji wenye tija ikiwa ni pamoja na kutumia mtandao mpana wa Shirika la Posta ambao una matawi zaidi ya 350 yaliyosambaa nchi nzima, bara na visiwani.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji amesema Umoja wa Posta duniani ni chombo cha Umoja wa Mataifa (UN) chenye jukumu la kuendeleza huduma za Posta hapa duniani ambapo ifikapo Oktoba 9 kila mwaka, Tanzania kama mwanachama wa Posta duniani aliyejiunga mwaka 1963, huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ambayo umoja  huu ulianzishwa mwaka 1874.

“Katika mkutano mkuu wa Umoja wa Posta Duniani Tanzania iifanikiwa kushika nyadhfa za uongozi kwenye viti vya ujumbe katika mabaraza yote mawili ya umoja huo, yani Baraza la Utawala (Council of Administration) na Baraza la uendeshaji la Posta (Postal Operations Council),”amesema na kuongeza kuwa

“Katika kusherehekea siku hii ,Tanzania tumefanya  maadhimisho haya kwa siku nne mfululizo na kushirikisha wadau mbalimbali katika Sekta ya Posta na nje ya Sekta ya Posta kwa lengo la kuonesha umma umuhimu wa huduma za Posta nchini.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  Rahma Kassim Ali amesema,ametoa pongezi kwa Umoja wa Posta Duniani kwa kufikisha miaka 147 tangu kuanzishwa kwake.

Katika maadhimisho hayo Dkt.Mpango amekabidhi magari 18 na pikipiki 20 kwa shirika la Posta ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi kwa urahisi.

Pia katika kilele cha maadhimisho Dkt.Mpango amekabidhi  vyeti na tuzo kwa wadau na washiriki wa uandishi wa insha kuhusu matumizi ya huduma mpya ya kidigitali zinazotolewa na shirika hilo.