Na Mwandishi Wetu,Timesmajira, Kibondo
MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango ameshiriki mazishi ya marehemu John Tutuba ambaye ni Baba mzazi wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Emmanuel Tutuba yaliyofanyika kijijini kwake Kibondo mkoani Kigoma leo.
Mazishi hayo yametanguliwa na Ibada ya kuaga mwili wa marehemu
iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Maria Mama wa Mungu Wilayani Kibondo na kuongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma Mhashamu Askofu Joseph Mlola.
Akitoa salamu za rambirambi, Makamu wa Rais alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali nzima wanaungana na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Makamu wa Rais amesema marehemu mzee John Tutuba alikuwa mtumishi mwaminifu wa umma katika nafasi zote alizowahi kuzitumikia enzi za uhai wake.
Amesema pia aliwatunza vyema watoto wake katika maadili na
kuhakikisha wanapata elimu na hivyo kutumika kulisaidia Taifa.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kujenga tabia ya kuhakikisha watoto wao wanapata elimu itakayowasaidia wao na Taifa kwa ujumla.
Aidha amewasihi Watanzania kutimiza wajibu wao katika jamii ikiwemo kuwaenzi na kuwatunza wazazi na walezi wao pindi wanapohitaji msaada.
Makamu wa Rais ametoa wito wa kuwajenga watoto katika maadili mema yatakayoanzia katika imani za dini.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu