Na Mwandishi wetu, Timesmajira, Online
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasili nchini Rwanda kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Heads of Government Meeting-CHOGM) unaofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kigali.
Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo ulioanza Juni 20 na unatarajia kuhitimishwa Juni 25,2022.
Makamu wa Rais, mbali ya kushiriki kwenye mkutano huo ameombwa pia miadi ya kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Namibia, Hage Geingob; Waziri Mkuu wa Mauritius; Pravind Jugnauth; Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau na Melinda Gates.
Inaelezwa kuwa miadi hiyo ni ishara ya dhahiri ya kuendelea kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania duniani chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia. Hivyo, Makamu wa Rais anatarajiwa kutumia miadi hiyo kusisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande mbili na hasa ushirikiano katika eneo la uwekezaji na biashara pamoja na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula naye yupo nchini humo kushiriki Mkutano huo katika ngazi ya Mawaziri Juni 23,2022. Kama ilivyo kwa Makamu wa Rais, Balozi Mulamula ameombwa miadi ya kufanya mazungumzo na Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za India, Zambia, Botswana, Eswatini, Singapore na mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, Bibi Cherie Blair ambaye ni mwanzilishi wa Cherie Foundation.
Wakati huo huo, mikutano ya utangalizi ya mkutano huo, inaendelea ambapo tarehe 20 hadi 23 Juni 2022 ilifanyika mikutano ya jukwaa la vijana, jukwaa la wanawake na jukwaa la biashara. Tanzania ilishiriki katika majukwaa yote hayo
Wakati wa mkutano wa jukwaa la biashara, washiriki pamoja na mambo mengine, walijadili namna bora ya kufanya biashara huku dunia ikiwa bado inakabiliwa na janga la ugonjwa wa Corona na athari za vita kati ya Urusi na Ukraine.
Ujumbe wa Tanzaia katika mkutano huo uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah ambaye ameeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita za kuboresha mazingira ya biashara na fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Kwa upande wa mkutano wa jukwaa la vijana ambapo Tanzania iliwakilishwa na vijana saba, umesistizwa umuhimu wa kuwaendeleza vijana. Ilielezwa kuwa endapo nchi za Jumuiya ya Madola zinahitaji kufikia maendeleo ya kweli, hazina budi kuwekeza kwa vijana kwa sababu katika nchi hizo vijana ni zaidi ya asilimia 60.
Kuhusu mkutano wa jukwaa la wanawake, ulisisitizwa umuhimu wa kumuendeleza mwanamke ikiwa ni pamoja na kumpatia elimu ya kumiliki, kukuza na kufanya biashara, kuweka usawa wa kijinsia na kukomesha vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.
More Stories
Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA
Mwanafunzi apoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba