Na Joyce Kasiki,Timesmajira Online,Dodoma
MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango ametembelea wafiwa wa ndugu wa marehemu watano wa familia moja waliouawa na kufungiwa ndani katika tukio lililotokea hivi karibuni katika kijiji cha Zanka wilayani Bahi Mkoani Dodoma huku akimuagiza IGP Simon Sirro kuhakikisha mauaji yanakoma nchi nzima na kuhakikisha wahalifu wa mauaji hayo wanapatikana ndani ya siku saba.
Aidha Dkt.Mpango ambaye amefika kwa familia ya wafiwa kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan ,ametoa maelekezo kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama mkoani Dodoma kuhakikisha vinafanyia kazi suala hilo la mauaji na kuwasilisha taarifa yao ndani ya siku saba kwa Rais Samia.
Akizungumza wakati akiwafariji wafiwa hao Dkt.Mpango ameshangazwa kutokea kwa mauaji hayo na marehemu kukaa siku tatu na kuharibia ndani bila majirani wala uongozi wa kijiji kutokuwa na taarifa .
“Nimefika hapa kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kuja kutoa pole kwa familia ambayo imekatiliwa sana kwa kuuawa kwa watoto wao,lakini kutoa pole kwa kijiji cha Zanka na vijiji vyote vya jirani,poleni sana,
“Kwa kweli mheshimiwa Rais amesononeka sana,tukio hili ni la kikatili,la kinyama linaloleta maswali mengi, maana wazee hawa baba na mama itachukua miaka mingi machozi yao kukauka ,amesema na kuongeza kuwa
“Nataka niwaombe kwanza familia zetu zote katika kata hii ya Zanka na nchini kote ,watanzania tuna sifa duniani ya kupendana inakuwaje mwanafamilia haonekani siku tatu na wanafamilia wapo karibu ,hata hodi nyumba hii hakuna ,kuna tatizo kubwa,majirani kimya kabisa,yaani hata kushtuka, mbona jirani haonekani,kuna shida,uongozi wa mtaa,nyumba kumi,kijiji kimya kabisa mpaka mwili wa binadamu unaharibika ndio tunashtuka kweli,
“Nawasihi sana wanazanka wenzangu,wananchi wote nchini nzima lazima tupendane tujuliane hali ,pale ambapo pana matatizo hata kimila tukae tuzungumze kama wakatili wauaji hawa wanatoka vijiji jirani utaratibu wetu mgeni anapoingia kijijini anatolewa taarifa kwa uongozi.”
Dkt.Mpango amewataka viongozi kuanzia ngazi ya ubalozi kufuatilia maisha ya wananchi huku akiwaasa viongozi wa dini kwenye nyumba za ibada kuwakumbusha wananchi kwamba hakuna binadamu mwenye haki ya kuondoa uhai wa mtu mwingine .
“Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dodoma ,nifikishie salam kwa IGP ,mauaji haya nchi nzima yakome,mfanye kazi ya kuyazuia,polisi mna kazi kubwa ya kufanya nchi nzima ,Rais Samia na mimi tumechoka hatuwezi kuongoza yenye mauaji namna hii,
Ameitaka Idara ya Upelelezi ya mkoa wa Dodoma ihakikishe saa 24 inafanya kazi kuhakikisha wanapatikana huku akiwasihi wananchi kujenga mahusiano ya kuwa wanajuliana hali kila siku na kila wakati ili kugundua mapema matukio kama hayo.
Aidha amemtaka mwenyekiti wa mtaa huo kwa kushirtiukiana na Mkuu wa Wilaya ya Bahi afanye mikutano ya wananchi ili waelezane kuhusu usalama wa wananchi na mali zao.
Katika kijiji cha Zanka kata ya Zanka wilayani Bahi,Januari 22 yalitokea mauaji ya ndugu watano wa familia moja yaliyofanywa na watu wasiojulikana na marehemu hao kubainika kwamba wamekufa baada ya siku tatu huku miili yao ikiwa imeshaanza kuharibika.
More Stories
Asilimia 93 wananchi Ngombo wamelipwa fidia
Bei za mafuta zaendelea kushuka
RPC Mbeya:Jeshi la Polisi tupo timamu kuhakikisha wananchi wanasherekea mwaka mpya kwa amani