May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mpango ataka shule zote kuwa na walimu wa michezo

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAKAMU wa Rais Dkt Phillip Isdor Mpango amezindua mashindano ya taifa ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi (UMITASHUMTA) na shule za sekondari (UMISSETA) Mjini Tabora na kuagiza kila shule kuwa na Mwalimu wa michezo.

Alisema serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa kwenye sekta hii ikiwemo kuboreshwa miundombinu ya michezo katika shule mbalimbali ili kuinua sekta hiyo.

Alibainisha kuwa Mheshimiwa Rais ana dhamira ya kuendelea kuboresha zaidi michezo katika shule zote ili kuhakikisha Taifa linapiga hatua kubwa katika sekta hiyo ikiwemo kuinua vipaji vya wana michezo.

Dkt Mpango alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zozote zinazofanywa na wadau katika kuinua na kuimarisha sekta nzima ya michezo hapa nchini ili kuwezesha wanamichezo kutimiza ndoto zao.

Ili kufikia malengo hayo aliagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha kila shule ya msingi na sekondari inakuwa na mwalimu angalau mmoja wa michezo ili kuimarisha michezo na kuiendesha kitaaluma.

Aidha aliwataka kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanalindwa ili kutoa fursa kwa vijana kupata sehemu za kufanyia mazoezi ya ili kukuza vipaji vyao.

Alisisitiza kuwa maandalizi ya wachezaji mahili huanza katika umri mdogo hiyo ndio sababu ya kuwepo kwa mashindano haya ya Umitashumta na Umisseta ili kuibua mapema vipaji vyao na kuviendeleza.

Dkt Mpango alisema tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassani aingie madarakani ameleta hamasa kubwa kwa wanamichezo na ametenga fedha nyingi ili kuinua zaidi sekta hiyo.

Aidha aliagiza shule zote zinazojengwa kuwa na viwanja vya michezo, kuimarisha na kuboresha usafi wa mazingira ikiwemo kupanda miti kupendesha mazingira yake.

Kwa kutambua mchango na kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua sekta hiyo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hivi karibuni limemtunuku tuzo maalumu ya michezo.

Wakati huo Makamau wa Rais amezipongeza shule za serikali zilizoonyesha uwezo mkubwa na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alitaja shule hizo kuwa ni Kilombero ya Mkoani Morogoro walioibuka mabingwa katika mashindano ya Kanda ya 5 ya Afrika kwa michezo ya mpira wa mikono kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kwa 2023.

Nyingine ni shule ya msingi Mkalapa ya wasichana ya Mkoani Mtwara iliyoibuka kidedea katika mchezo wa wavu kwenye mashindano ya Afrika Mashariki (FEASSSA) yaliyofanyika jijini Arusha Septemba 2022, na shule ya Benjamin Mkapa ya Dar-es-salaam iliyoshiriki mashindano ya soka kanda ya CECAFA.

Makamu wa Rais aliitaka jamii kutambua na kuthamini sekta kwa kuwa ni fursa nzuri ya kupata ajira kwa vijana ikiwemo kutangaza nchi na kukuza sekta hiyo, huku akiwataka wananchi wote kujenga utamaduni wa kushiriki kwenye michezo au kufanya mazoezi.